Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa kushirikiana na MKA Foundation kutoka Uholanzi, inaendesha kambi maalumu ya upasuaji kwa wagonjwa wenye saratani na matatizo mengine yanayohusisha uso, kinywa, taya na shingo, huku wataalam wa MNH wakipata mafunzo ya nadharia na vitendo kwa lengo la kuimarisha ujuzi wao katika eneo hilo la kibingwa na kibingwa bobezi.Akizungumza leo mara baada ya upasuaji, Dkt. Baraka Kileo, Bingwa wa Upasuaji wa Uso, Kinywa na Taya MNH, amesema kambi hiyo itaendelea hadi tarehe 23 Oktoba 2026, inalenga kuwafikia wagonjwa zaidi ya 40, ambapo hadi sasa wagonjwa 32 wamefanyiwa uchunguzi wa awali na 15 kati yao wamefanyiwa upasuaji.
“Natoa pongezi kwa Serikali kwa uwekezaji unaofanyika katika sekta ya afya na kwa wadau wanaoshirikiana nasi. Kupitia ushirikiano huu, tunapata fursa ya kuimarisha utaalamu wetu na kuboresha huduma kwa wagonjwa ambao awali walilazimika kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu,” amesema Dkt. Kileo.
Kwa upande wake, Dkt. Abas Mugira, Bingwa wa Upasuaji wa Uso, Kinywa na Taya MNH ambaye ni mnufaika wa mafunzo hayo, amesisitiza umuhimu wa wananchi kutambua mapema dalili zinazoweza kuashiria saratani ya kinywa, uso na shingo, zikiwemo vidonda mdomoni visivyopona ndani ya wiki mbili, uvimbe usio wa kawaida na mabadiliko yanayoendelea katika maeneo hayo.
Aidha, Bw. Ismail Hussein ameishukuru MNH kwa huduma za matibabu alizopata, akieleza kuwa amekuwa akisumbuliwa na saratani ya shingo kwa takribani mwaka mmoja. Ameeleza kuwa kupata huduma katika hospitali hiyo kumempa fursa ya kufanyiwa uchunguzi na kupata matibabu yanayolenga kukabiliana na tatizo lake la kiafya, huku akiwashukuru madaktari, wauguzi na wataalam wengine wa afya kwa juhudi zao katika kumhudumia na kuwahimiza wananchi wenye changamoto za kiafya kufika hospitalini mapema kwa uchunguzi na matibabu stahiki.


No comments:
Post a Comment