JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


UFADHILI WA GEF WACHOCHEA UKUAJI WA UTALII WA MISITU TANZANIA

Share This

 Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM: Idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi za misitu nchini imeongezeka kutoka chini ya 200 mwaka 2015 hadi zaidi ya 390,000 kwa mwaka, mafanikio yanayohusishwa kwa sehemu na miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF).

Ukuaji huo unaashiria hatua muhimu katika juhudi za Tanzania kupanua vivutio vya utalii nje ya hifadhi za wanyamapori, kuongeza thamani ya kiuchumi ya rasilimali za misitu na kuimarisha uhifadhi endelevu.
Akizungumza katika mazungumzo ya kitaifa kuhusu awamu ya tisa ya ufadhili wa GEF (GEF-9), Mhifadhi Mwandamizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Yusuph Tango, ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa NETZERO unaofadhiliwa na GEF-8, alisema miradi iliyofadhiliwa na mfuko huo imechangia kuimarisha usimamizi wa baadhi ya misitu na kuwezesha kuendelezwa kwa shughuli za utalii katika hifadhi za misitu ya asili.

Tango alisema utalii wa misitu ulikuwa bado haujaimarika mwaka 2015, wakati idadi ya watalii waliotembelea hifadhi hizo ilikuwa chini ya 200 kwa mwaka, licha ya Tanzania kuwa na utambulisho mkubwa kimataifa katika utalii wa wanyamapori. Ufadhili huo pamoja na jitihada zingine za serikali zimesaidia kuongeza kwa idadi ya watalii kufikia takriban 400,000 mwaka 2025.

Alieleza kuwa kuboreshwa kwa hadhi na usimamizi wa baadhi ya maeneo ya misitu, pamoja na kutambuliwa kwake kama hifadhi za misitu ya asili, kumewezesha kuendeleza shughuli za utalii sambamba na uhifadhi wa bioanuai.

Alisema TFS imekuwa ikinufaika na ufadhili wa GEF tangu mwaka 2007 kupitia awamu mbalimbali, zikiwamo GEF-4, GEF-5 na GEF-6, na sasa inaangalia fursa mpya katika GEF-9 ili kuimarisha zaidi uhifadhi na kuendeleza shughuli za utalii katika hifadhi za misitu na nyuki.

Tango alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na wadau kuandaa mapendekezo ya miradi yanayozingatia vipaumbele vya mazingira vya Tanzania na malengo ya ufadhili wa GEF, akieleza kuwa msaada zaidi unaweza kuongeza mchango wa rasilimali za misitu na nyuki katika maendeleo ya taifa.

Mazungumzo ya GEF-9 yanawakutanisha wadau kujadili fursa za ufadhili, kujifunza kutokana na miradi iliyopita na kuweka vipaumbele vya miradi mipya itakayochangia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa bioanuai, uharibifu wa ardhi na uchafuzi wa mazingira.


























No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad