Na Mwandishi Wetu, Dar
MKUTANO Mkubwa wa Sita wa Kimataifa wa Ubora wa Elimu, (International Quality Education Conference -IQEC 2026), unatarajia kufanyika Novemba 11 hadi 13, 2026, jijini Dar es Salaam, huku ukiwakutanisha wadau anuai wa elimu Afrika na sehemu mbalimbali duniani.
Akizungumzia Mkutano huo, Mratibu Taifa wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Martha Makala amesema mkutano huo muhimu utakaojadili na kuhamasisha maamuzi na hatua madhubuti za upatikanaji wa rasilimali za kutosha na endelevu kwa ajili ya sektya ya elimu unatarajia kukutanisha takribani washiriki 500 kutoka nchi zisizopungua 20.
"...Mkutano huu unalenga kuhamasisha maamuzi na hatua madhubuti za kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali za kutosha na endelevu kwa ajili ya sektya ya elimu, hususan kupitia uhamasishaji wa rasilimali za ndani na kuimarisha ushirikiano wenye ufanisi na endelevu kati ya sekta binafsi na Serikali," alisema Bi. Makala akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.
Alibainisha kuwa kupitia jukwaa hilo la elimu, Afrika inaweza kujenga mfumo wa elimu bora, jumuishi na endelevu kwa kuwekeza rasilimali za ndani za kutosha, kupanga matumizi yake kwa ufanisi na kuhakikisha kuwa kila senti inayotengwa kwa elimu inaleta matokeo yanayoonekana kwa wanafunzi na walimu.
Aidha Mratibu huyo wa TEN/MET aliyataja mataifa ambayo yanatarajia kushiriki katika mkutano wa IQEC 2026 kuwa ni pamoja na Marekani, Uingereza, Norway, Brazil, India, Australia, Syria Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda, Zimbabwe, Zambia, Afrika Kusini, Malawi, Botswana, na Nigeria.
Aliongeza kuwa washiriki wa mkutano huo, watajumuisha watunga sera, viongozi na taasisi za Serikali, wadau wa maendeleo, mashirika ya kiraia, wataalamu na watafiti wa elimu, vyuo vikuu, sekta binafsi, walimu, wanafunzi, waandishi wa habari, vijana na wadau wengine wa maendeleo.
"Kimsingi hili ni jukwaa muhimu sana katika sekta ya elimu la kubadilishana uzoefu, kujadili tafiti mbalimbali na kuchakata mbinu bora zinazoweza kusaidia Tanzania na Afrika kwa ujumla kuimarisha uhusiano baina ya Serikali na sekta binafsi kujenga mfumo wa upatikanaji wa rasilimali za elimu ulio endelevu na usiotegemea kwa kiwango kikubwa vyanzo vya nje ambavyo vinaweza kubadilika kutokana na mazingira na vipaumbele vya kimataifa," alisisitiza Bi. Martha Makala.
IQEC 2026 ni jukwaa la kuwakutanisha wadau wa elimu kutoka Tanzania, Afrika na sehemu mbalimbali duniani ili kubadilishana mawazo, ubunifu, tafiti na uzoefu kuhusu afua zenye matokeo chanya katika kuboresha elimu.
Elimu ni msingi wa maendeleo ya Taifa. Inawezesha vijana kupata maarifa na ujuzi, inakuza ubunifu na tija, inachochea ukuaji wa uchumi na inaliandaa Taifa kukabiliana na changamoto za sasa na zijazo. Tanzania imepiga hatua muhimu katika kupanua upatikanaji wa elimu kupitia uwekezaji wa Serikali katika miundombinu, utekelezaji wa elimu bila ada na maboresho ya sera na mifumo ya elimu ikiwemo Sera ya Elimu ya 2014 toleo la mwaka 2023. Hatua hizi ni muhimu sana na zinapaswa kupongezwa na kuendelezwa.



No comments:
Post a Comment