JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


NDEJEMBI ATAJA VIPAUMBELE SITA COP12

Share This

 

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Deogratius John Ndejembi, ametaja vipaumbele sita vinavyopaswa kupewa uzito na nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi ili kuimarisha uhifadhi wa mazingira ya bahari na kukuza uchumi endelevu wa buluu katika ukanda wa Bahari ya Hindi ya Magharibi.

Dkt. Ndejembi amesema vipaumbele hivyo ni kutekeleza Mkataba wa Nairobi na itifaki zake kupitia sheria, taasisi na bajeti za kitaifa; kuimarisha hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi; kuongeza mapambano dhidi ya uchafuzi wa bahari; kulinda bioanuwai huku uwekezaji ukiongozwa kwa uwajibikaji; kuwekeza katika sayansi, takwimu na fedha endelevu; pamoja na kuwashirikisha kikamilifu sekta binafsi, wanawake na vijana.

Akifungua Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12) leo Oktoba 8, 2026 jijini Dar es Salaam, Dkt. Ndejembi amesema utekelezaji wa vipaumbele hivyo ni muhimu katika kuifanya miaka 40 ijayo ya mkataba huo kuwa kipindi cha hatua madhubuti za kulinda bahari na kuboresha maisha ya jamii za pwani.

Amesema nchi wanachama zinapaswa kuhakikisha maazimio ya mkataba, itifaki na mikutano ya nchi wanachama yanatafsiriwa kuwa sheria, taasisi, bajeti na mifumo ya utekelezaji, huku ikiwekwa mifumo ya wazi ya kupima na kuripoti maendeleo na changamoto.

Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, amesema nchi hizo zinapaswa kuharakisha urejeshwaji wa mikoko, nyasi bahari na miamba ya matumbawe, kukabiliana na ongezeko la tindikali baharini na kuhakikisha masuala ya bahari yanaingizwa katika mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Ndejembi amesema uchafuzi wa bahari nao unahitaji hatua za pamoja, ikiwemo kudhibiti taka za plastiki, kemikali na maji taka kupitia mfumo unaounganisha vyanzo vya uchafuzi hadi baharini, pamoja na kuimarisha maandalizi ya kikanda kukabiliana na majanga makubwa ya baharini.

Amesema kulinda bioanuwai kunapaswa kwenda sambamba na uwekezaji unaowajibika, akisisitiza matumizi ya mipango ya matumizi ya maeneo ya bahari, tathmini za mifumo ya ikolojia na maeneo ya uhifadhi katika kuongoza shughuli za uvuvi, bandari, utalii na nishati.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika utafiti, akili bandia (AI), ufuatiliaji, takwimu zinazoshirikishwa na taasisi za utafiti na elimu, pamoja na kuongeza upatikanaji wa fedha endelevu kwa ajili ya miradi ya uhifadhi na uchumi wa buluu.

Amesema sekta binafsi, wanawake na vijana wanapaswa kuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa ajenda hiyo, akifurahishwa na kuanzishwa kwa mara ya kwanza katika COP12 kwa Jukwaa la Biashara, Jukwaa la Vijana na ushiriki wa wanawake, akitaka utaratibu huo uwe wa kudumu katika mikutano ijayo ya nchi wanachama.

Wakati huo huo, Aidha Kaimu Katibu Mkuu Msaidizi wa Umoja wa Mataifa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Elizabeth Mrema, alizitaka nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi kutumia jukwaa hilo kugeuza ahadi za kimataifa kuhusu mazingira kuwa hatua zinazotekelezeka katika Bahari ya Hindi ya Magharibi.

Mrema alisema hatua hiyo ni muhimu wakati eneo hilo likikabiliwa na changamoto zinazohusisha mabadiliko ya tabianchi, kupotea kwa viumbe hai na uchafuzi wa mazingira, ambazo zinahitaji ushirikiano wa nchi kwa kuwa haziwezi kutatuliwa na taifa moja.

 







No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad