.jpeg)
Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, ameutaka Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12) kuhakikisha maamuzi yatakayofikiwa yanaelekeza hatua za utekelezaji na kuleta matokeo halisi katika maeneo ya pwani na bahari, badala ya kuishia katika ahadi zisizotekelezeka.
Masauni alitoa msisitizo huo leo Oktoba 10, 2026 wakati wa Mkutano wa Watendaji Wakuu na Washirika wa COP12, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Alisema wajumbe wanapaswa kuhakikisha ripoti, tathmini na rasimu za maamuzi zinaonyesha hali halisi ya utekelezaji, mafanikio yaliyopatikana, mapungufu yaliyopo na hatua za pamoja zinazohitajika.
“Jukumu lenu si kurekodi shughuli pekee. Ni kubaini nini kimebadilika, wapi utekelezaji unaendelea, wapi kuna mapungufu na ni hatua gani za pamoja zinazohitajika,” alisema.
Masauni alisema rasimu za maamuzi zinapaswa kulenga utekelezaji na kila hatua inayopendekezwa iwe na madhumuni yaliyo wazi, mhusika anayehusika, utaratibu wa utekelezaji na msingi wa kufuatilia maendeleo.
“Maamuzi ambayo hayawezi kutafsiriwa kuwa hatua za kitaifa na kikanda hayatakidhi uharaka uliopo mbele yetu,” alisema.
Alisema nchi wanachama zinapaswa kulenga maamuzi machache, yaliyo wazi na yenye matokeo zaidi badala ya kuongezeka kwa ahadi zenye nia njema lakini zisizotekelezeka.
“Tunapaswa kulenga maamuzi machache, yaliyo wazi na yenye matokeo zaidi badala ya kuongezeka kwa ahadi zenye nia njema lakini zisizotekelezeka,” alisema.
Masauni alisema mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kupasha joto na kuongeza tindikali katika maji, hali inayotishia miamba ya matumbawe na uvuvi, pamoja na maisha ya jamii za pwani na uchumi wa kitaifa.
Alisema uchafuzi wa plastiki unaathiri pwani na bahari, huku matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali yakipunguza akiba ya samaki na kuharibu maeneo ya makazi ya viumbe baharini.
“Mahitaji ya rasilimali za bahari yanaongezeka na shinikizo katika mifumo yetu ya ikolojia ya bahari na pwani linaongezeka,” alisema.
Alisema Tanzania, katika kipindi cha uongozi wake wa Ofisi ya Mkataba wa Nairobi, imesimamia hatua mbalimbali muhimu, zikiwemo kukamilishwa na kupitishwa kwa Itifaki ya Anuwai ya Bahari na Pwani na Maeneo Yaliyohifadhiwa, Mpango wa Kikanda wa Dharura za Mafuta na Mkakati wa Kikanda wa Plastiki na Kemikali Zinazohusiana.
Pia alisema Tanzania imeanza kuandaa Dira na Mfumo wa Utekelezaji wa Kikanda wa BBNJ, huku baadhi ya mifumo hiyo ikitarajiwa kujadiliwa na kupitishwa katika COP12.
Masauni alisema changamoto za mazingira zinahitaji majibu yanayounganisha ulinzi na urejeshaji wa mifumo ikolojia na mahitaji ya watu, ikiwamo usalama wa chakula, miundombinu inayostahimili changamoto na shughuli za kiuchumi zinazowajibika.
“Mtazamo huu jumuishi ndio msingi wa uchumi endelevu wa buluu na lazima uonekane katika maamuzi yetu,” alisema.
Alisisitiza pia ushirikishwaji wa jamii za pwani, wanawake na vijana katika sera na uwekezaji unaoathiri maisha yao, akisema hawapaswi kuwa wanufaika pekee bali pia mawakala wa mabadiliko.
“Thamani ya Mkataba huu itapimwa kwa matokeo yaliyopatikana katika maeneo yetu ya pwani na bahari, na si kwa idadi ya mikutano iliyofanyika au maamuzi yaliyopitishwa,” alisisitiza.
Masauni alisema maamuzi yatakayofikiwa katika COP12 yataathiri afya ya bahari na ustawi wa watu kwa miongo ijayo, hivyo wajumbe wanapaswa kuwa na mtazamo wa kimkakati, shirikishi na wa kuangalia mbele.

.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)



No comments:
Post a Comment