Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa majengo mapya ya Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ya juu kupitia uwekezaji wa kimkakati unaolenga kupanua fursa za elimu, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya maendeleo ya taifa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Rais amesema Serikali, kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, imewekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 425, sawa na takribani shilingi trilioni moja, katika kuimarisha elimu ya juu nchini kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), huku Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa kikinufaika na uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 30.
Amesema uwekezaji huo ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha ongezeko la wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi na sekondari linaendana na upatikanaji wa nafasi za elimu ya juu, akibainisha kuwa tangu mwaka wa fedha 2021/2022, Mkoa wa Iringa umepokea zaidi ya shilingi bilioni 175 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu katika ngazi hizo.
Katika kuhakikisha uwekezaji huo unaleta matokeo yaliyokusudiwa, Mheshimiwa Ndejembi ameuagiza uongozi wa Chuo hicho kusimamia kwa umakini, uwazi na uadilifu fedha zote zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa kukamilisha ujenzi kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora. Amesema Serikali haitavumilia matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma, kwani kila shilingi inayowekezwa katika elimu inapaswa kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa Watanzania.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda, akizungumza wakati wa kumkaribisha Makamu wa Rais, ameipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanya uwekezaji mkubwa na wa kihistoria katika sekta ya elimu ya juu, akieleza kuwa kupitia Mradi wa HEET, jumla ya Taasisi 20 za elimu ya juu nchini zimenufaika na ujenzi wa maabara 309, hosteli 26, maktaba, kafeteria na ofisi 1,177, pamoja na ukarabati wa majengo 48, hatua inayofungua ukurasa mpya katika kuboresha mazingira ya ufundishaji, ujifunzaji, tafiti na ubunifu nchini.
Profesa Mkenda amesema mafanikio hayo hayaishii katika ujenzi wa majengo pekee, bali yameambatana na upanuzi wa wigo wa elimu ya juu kwa kuanzishwa kwa kampasi mpya katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo mikoa ya Manyara, Kagera, Lindi, Njombe, Katavi, Kigoma, Mwanza, Rukwa, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Tanga, Singida, Mara na Ruvuma pamoja na Zanzibar. Amesema hatua hiyo inalenga kusogeza huduma za elimu ya juu karibu na wananchi, kupunguza changamoto ya umbali na gharama za masomo, pamoja na kutoa fursa zaidi kwa vijana kupata elimu na ujuzi utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa Taifa.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa, amesema chuo hicho kimeendelea kupiga hatua kubwa katika kuimarisha miundombinu ya elimu kupitia utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa majengo saba yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 30.4, inayojumuisha majengo ya sayansi, maabara ya fizikia, midia anuwai na elimu maalumu, hosteli za wanafunzi pamoja na maktaba. Ameeleza kuwa hadi kufikia Septemba 30, 2026, ujenzi wa majengo manne yanayofadhiliwa kupitia Mradi wa HEET ulikuwa umekamilika kwa asilimia 100, hatua inayotarajiwa kuongeza uwezo wa chuo kupokea wanafunzi wengi zaidi na kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa.
Mkwawa ni miongoni mwa vyuo muhimu vinavyoandaa walimu wa sayansi na masomo mengine hapa nchini. Kuongezeka kwa mabweni, maabara na madarasa ya kisasa kutaongeza idadi ya wanafunzi wanaoweza kudahiliwa na kuimarisha mafunzo ya vitendo kwa walimu watakaofundisha vizazi vijavyo


.jpeg)



.jpeg)



.jpeg)



No comments:
Post a Comment