JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Benki ya Absa yatoa wito kwa Wanawake kutumia maarifa ya kifedha kujiwezesha kiuchumi

Share This
Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam


WANAWAKE wametakiwa kuimarisha uelewa wao kuhusu masuala ya kifedha na uwekezaji, mambo yatakayowasaidia kuongeza kipato na akiba, hivyo kuwawezesha kuwa na uhuru kamili wa kifedha.

Wito huo ulitolewa wakati wa semina ya elimu ya kifedha kwa wanawake iliyopewa jina la “Road to Financial Freedom”, iliyoandaliwa na Accelerate Women na kudhaminiwa na Benki ya Absa Tanzania jijini Dar es Salaam jana.

Semina hiyo iliwakutanisha wanawake wajasiriamali kujadili masuala mbalimbali ya elimu ya fedha, akiba, uwekezaji na matumizi sahihi ya huduma za kifedha, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukuza uhuru wa kifedha miongoni mwa wanawake.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Bidhaa Kitengo cha Biashara wa Benki ya Absa Tanzania, Bi Devroda Kagusa, alisema upatikanaji wa huduma za kifedha unapaswa kwenda sambamba na uelewa wa kutosha wa masuala ya fedha ili kuwawezesha wanawake kufanya maamuzi sahihi kuhusu fedha zao.

“Absa tunajivunia kuunga mkono matukio kama haya. Tukio la leo linatoa fursa kwa wanawake kujifunza, kupata taarifa na kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi ya huduma za kifedha zinazoweza kuimarisha ushiriki wao katika mfumo rasmi wa kifedha,” alisema.

Bi Devroda alisema msaada wa benki kwa mpango huo ni sehemu ya dhamira yake ya kuendeleza ujumuishaji wa kifedha nchini, akiongeza kuwa mpango huo pia unaendana na ahadi ya chapa ya Absa isemayo “Stori yako ina Thamani”.

Alisema wanawake wanaweza kusogea karibu zaidi na uhuru wa kifedha kwa kujenga uwezo wa kusimamia fedha zao kwa ufanisi na kutumia huduma zinazofaa za kifedha kwa mahitaji yao binafsi na ya biashara.

“Absa imejitolea kikamilifu na inatiwa moyo na mipango kama hii inayowapa wanawake fursa ya kujifunza kuhusu huduma za kifedha zinazoweza kuwawezesha kusimamia na kuchukua udhibiti wa masuala yao ya kifedha, sisi Absa kila Stori ya mafanikio ina thamani sana kwetu” alisema.

Bi Devroda pia alitaja SHE Account ya Absa, akisema ni miongoni mwa huduma za benki zilizoundwa kwa kuzingatia mahitaji maalumu ya kifedha ya wanawake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Accelerate Women, Bi Bernice Fernandes, alisema ukosefu wa uelewa kuhusu uwekezaji ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wanawake wanaotaka kukuza rasilimali zao za kifedha.

“Jambo hili ndilo lililotufanya tuamue kuandaa semina hii. Mafunzo haya yanatoa jukwaa ambalo wanawake wanaweza kupata maarifa yanayowawezesha kufanya maamuzi sahihi, kuweka akiba kwa ufanisi na kuwekeza kwa busara,” alisema.

Bi Bernice alisema kufanya maamuzi bora ya kifedha kunaweza kuwasaidia wanawake kujenga msingi imara wa kifedha na wakati huo huo kuchangia katika ukuaji wa uchumi kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Accelerate Women, Bi Monica Hangi, alisema wanawake wengi wana fedha lakini hawana uelewa wa kutosha kuhusu mahali sahihi pa kuwekeza ili kupata faida na kukuza mitaji yao na hatimaye kupata na uhuru wa kifedha.

Alisema kuongeza uelewa kuhusu uwekezaji ni muhimu katika kuwawezesha wanawake kutumia fedha zao kwa tija na kujenga maisha bora ya kifedha kwa muda mrefu.
Meneja Bidhaa Kitengo cha Biashara wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Devroda Kagusa, akitoa mada kuhusu uwezeshaji wa wanawake katika masuala ya fedha wakati wa semina ya siku moja ya elimu ya fedha iliyopewa jina la “Road to Financial Freedom”, iliyoandaliwa na Accelerate Women na kudhaminiwa benki hiyo, jijini Dar es Salaam jana.

Meneja Msaidizi wa Uhakiki wa Biashara (Assistant Business Assurance Manager) wa Absa Bank Tanzania, Bi. Miriam Ngajilo, akitoa mada kuhusu ujumuishaji wa kifedha wakati wa semina ya siku moja ya elimu ya kifedha iliyopewa jina la “Road to Financial Freedom”, iliyoandaliwa na Accelerate Women na benki hiyo, jijini Dar es Salaam jana.



Meneja Bidhaa Kitengo cha Biashara wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Devroda Kagusa (wa pili kushoto), akisalimiana na Mkurugenzi wa Accelerate Women, Bi. Bernice Fernandes, wakati wa semina ya siku moja kuhusu elimu ya kifedha iliyopewa jina la “Road to Financial Freedom”, iliyoandaliwa na Accelerate Women na benki hiyo, jijini Dar es Salaam jana. Wengine ni baadhi ya wafanyakazi wa taasisi hiyo ya kifedha.


Mkurugenzi wa Accelerate Women, Bi. Bernice Fernandes (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Benki ya Absa Tanzania pamoja na washiriki wengine wa semina ya siku moja kuhusu elimu ya kifedha iliyopewa jina la “Road to Financial Freedom”, iliyoandaliwa na Accelerate Women na kudhaminiwa na Benkiy a Absa Tanzania, jijini Dar es Salaam jana.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad