JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Bandari SACCOS na Foundation Zapeleka Huduma za Uchangiaji Damu kwa Jamii

Share This
Na Mwandishi Wetu
BANDARI SACCOS, kwa kushirikiana na Bandari Foundation, imeendelea kuimarisha ushirikiano na jamii kupitia shughuli za uchangiaji damu, upimaji wa afya bila malipo na utoaji wa elimu ya afya. Shughuli hizo ni sehemu ya juhudi za kuboresha ustawi wa wananchi na kuwasaidia kupata huduma muhimu za kijamii.

Akizungumza katika viwanja vya Mwembeyanga jijini Dar Es Salaam leo Oktoba 26, 2026 kuhusu shughuli hizo, Mtendaji Mkuu wa Bandari SACCOS na mjumbe wa Bandari Foundation, Godfrey Rwehumbiza, amesema taasisi hizo zimejipanga kuhamasisha wananchi kujitokeza kuchangia damu, huku zikiendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa zoezi hilo, vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa na mchango wa uchangiaji damu katika kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.

Rwehumbiza amesema shughuli hizo pia zinahusisha upimaji wa afya bila malipo, kwa kushirikiana na wadau wa afya, wakiwamo Hospitali ya Bandari na Hospitali ya Temeke, ili kuwawezesha wananchi kufahamu hali zao za kiafya na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu.

Kwa upande wake, Juhudi Nyambuka amesema wananchi watapata elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, yakiwamo magonjwa ya moyo na kisukari, pamoja na umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza na kuchukua hatua stahiki mapema.

Nyambuka amesisitiza kuwa huduma hizo hazilengi watu wanaotaka kuchangia damu pekee, bali pia wananchi wanaohitaji kupima afya zao na kupata ushauri wa kitaalamu. Hivyo, amewahimiza wananchi kutumia fursa hiyo kujifunza zaidi kuhusu afya zao na namna ya kujikinga na magonjwa mbalimbali.

Aidha, amesema waandaaji wameweka utaratibu wa kufikisha huduma za uchangiaji damu katika maeneo mbalimbali ili kurahisisha upatikanaji wake. Taasisi, vikundi na maeneo yenye watu wasiopungua 10 wanaohitaji huduma hiyo yanaweza kutoa taarifa kwa waandaaji ili timu ya wataalamu ifike walipo na kutekeleza zoezi hilo.

Amesema utaratibu huo unalenga kuwafikia wananchi ambao wanaweza kushindwa kufika katika kituo kikuu cha shughuli hizo, huku akieleza kuwa huduma hizo zitapatikana katika maeneo yatakayopangwa kwa kushirikiana na waandaaji.

Kwa mujibu wa wazungumzaji hao, shughuli hizo zinatarajiwa kuendelea hadi Oktoba 19, huku wananchi wakihimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchangiaji damu na kutumia huduma za afya zinazotolewa.

Mbali na huduma za afya, Bandari SACCOS na Bandari Foundation zinaendelea kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kutoa elimu ya fedha kwa jamii. Wananchi pia watapata fursa ya kufahamu huduma na masharti ya kujiunga na Bandari SACCOS, ikiwa ni sehemu ya juhudi za taasisi hizo kuimarisha ustawi wa jamii.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad