NEW YORK, Marekani
TANZANIA imetangaza rasmi azma ya kuwania nafasi ya uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) kwa kipindi cha mwaka 2029–2030, ikiahidi kupeleka sauti imara ya Afrika na kusukuma mbele diplomasia ya kuzuia migogoro, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani na mageuzi ya operesheni za kulinda amani.
Msimamo huo umetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mjadala wa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaofanyika jijini New York, Marekani.
Mhe. Ndejembi amesema iwapo Tanzania itachaguliwa, itatoa kipaumbele kwa diplomasia ya kuzuia migogoro kabla haijageuka kuwa vita, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani, kuimarisha nafasi ya wanawake katika ulinzi na ujenzi wa amani, kuongeza ushiriki wa vijana katika ajenda ya amani na usalama, pamoja na kusukuma mbele mageuzi ya operesheni za Umoja wa Mataifa za kulinda amani.
Amesema azma hiyo imepata uungwaji mkono wa Umoja wa Afrika (AU), huku uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Usalama kwa kipindi hicho ukitarajiwa kufanyika Juni 2028.
TANZANIA YASISITIZA MAGEUZI UN
Katika hotuba hiyo, Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuendelea kufanyika kwa mageuzi katika Umoja wa Mataifa ili kuimarisha misingi ya haki, usawa na uwakilishi wenye uwiano, badala ya mfumo wa kimataifa kuendelea kuakisi zaidi nguvu na ushawishi wa mataifa machache.
Mhe. Ndejembi amesema mageuzi hayo ni muhimu zaidi katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na migogoro na vita, athari za mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya magonjwa, kasi ya maendeleo ya Akili Mnemba (AI) na changamoto za usalama wa nishati.
TANZANIA YAPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO
Akizungumzia afya ya mama na mtoto, Mhe. Ndejembi amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya mama na mtoto, ikiwamo kuongeza kiwango cha uzazi unaofanyika katika vituo vya afya kutoka asilimia 51 mwaka 2015 hadi asilimia 81 mwaka 2022.
Amesema uzoefu huo unaonesha kuwa uwekezaji katika miradi inayotekelezeka na inayoweka ustawi wa watu mbele unaweza kugeuza ahadi kuwa matokeo yanayoonekana na kupimika.
Kwa msingi huo, amesema Rais Samia Suluhu Hassan alikubali kuwa kinara wa masuala ya Afya ya Mama na Mtoto kwa niaba ya Umoja wa Afrika.
Mhe. Ndejembi amesema chini ya uongozi huo, Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama kwa asilimia 80 ndani ya kipindi cha miaka saba, akisisitiza kuwa nchi hiyo inalenga kufikia malengo ya “Sifuri Tatu” (Three Zeros).
Malengo hayo ni kutokuwepo kwa vifo vya mama na mtoto vinavyoweza kuzuilika, kutokuwepo kwa uzazi unaofanyika majumbani na kutokuwepo kwa watoto ambao hawajapata chanjo.
Amesema Afrika inaweza kufikia malengo hayo, lakini inahitaji uongozi thabiti wa kisiasa, rasilimali fedha za kutosha na ushirikiano imara zaidi kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.
TANZANIA YATAKA MAGEUZI YA MFUMO WA FEDHA DUNIANI
Tanzania pia imesisitiza umuhimu wa nchi zinazoendelea kupewa sauti kubwa zaidi katika taasisi na mifumo ya kimataifa inayofanya maamuzi ya kifedha yanayoathiri uchumi na maendeleo yake ya muda mrefu.
Mhe. Ndejembi amesema Tanzania imewasilisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kama msingi wa kujenga uchumi jumuishi, shindani na unaoweza kustahimili misukosuko, kupitia uwekezaji katika watu, miundombinu yenye tija, teknolojia, ubunifu, wanawake na vijana.
Amesema mageuzi katika mfumo wa fedha wa kimataifa ni muhimu ili nchi zinazoendelea ziweze kupata rasilimali zinazohitajika kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Ametaja umuhimu wa kuongeza mikopo yenye masharti nafuu, kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi, kurahisisha upatikanaji wa fedha za maendeleo na tabianchi, pamoja na kuongeza ushiriki wa nchi zinazoendelea katika maamuzi ya kifedha duniani.
TABIANCHI, NISHATI SAFI
Katika eneo la mabadiliko ya tabianchi, Tanzania imeeleza wasiwasi kuhusu pengo lililopo kati ya kiwango cha uzalishaji wa gesi chafuzi duniani na fedha zinazotolewa kusaidia nchi zinazoathirika kukabiliana na madhara yake.
Tanzania imesisitiza kuwa nchi zinazochangia kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa gesi chafuzi zinapaswa kubeba wajibu mkubwa zaidi katika kugharamia hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Katika mkakati wake wa mpito kuelekea nishati safi, Tanzania imetaja Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115, miradi ya nishati ya jua na upepo yenye jumla ya megawati 650, pamoja na mipango ya kuzalisha megawati 130 za nishati ya jotoardhi.
Pia, Tanzania imeeleza uwekezaji katika reli ya umeme na lengo la kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia hadi kufikia asilimia 80 ya kaya ifikapo mwaka 2034.
TANZANIA YAPINGA VIKWAZO VYA UPANDE MMOJA
Katika diplomasia ya kimataifa, Tanzania imepinga matumizi ya vikwazo vya upande mmoja vinavyowekwa na baadhi ya mataifa dhidi ya mataifa mengine, ikisema hatua hizo zinaweza kudhoofisha mamlaka ya nchi, kuathiri maendeleo na kupunguza uwezo wa wananchi kunufaika kikamilifu na haki zao.
Tanzania imeeleza mshikamano wake na Cuba, Zimbabwe na mataifa mengine yanayokabiliwa na vikwazo hivyo, huku ikitoa wito wa kuchukuliwa hatua za makusudi kuelekea kuondolewa kwa vikwazo bila masharti.
TANZANIA YATOA WITO WA AMANI GAZA
Kuhusu hali ya Gaza na Mashariki ya Kati, Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuwalinda raia, kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia wanaohitaji bila vikwazo na kurejesha diplomasia kuwa njia kuu ya kutafuta amani ya kudumu.
Kwa ujumla, ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umeunganisha ajenda ya maendeleo ya Taifa na hoja pana kuhusu nafasi ya Afrika katika mfumo wa kimataifa.
Tanzania imesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa haupaswi kuwa jukwaa linaloakisi pekee uwiano wa nguvu duniani, bali taasisi inayosimamia haki, mshikamano, usawa na maendeleo kwa mataifa yote.
Msimamo huo unaweka bayana ajenda ambayo Tanzania inalenga kuibeba katika safari yake ya kuwania nafasi ya uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2029–2030; kuimarisha sauti ya Afrika, kuzuia migogoro, kutetea suluhu za amani na kusukuma mageuzi ya mfumo wa kimataifa ili uwe na uwakilishi wenye uwiano zaidi.

.jpeg)

.jpeg)


No comments:
Post a Comment