JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


PSSSF Na Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) wajenga ushirikiano mkakati wa kuongeza elimu ya hifadhi ya jamii

Share This

 Dar es Salaam


Katika kile kinachoelezwa kuwa ni hatua madhubuti ya kupanua wigo wa utoaji wa elimu kwa umma, timu ya maofisa wa juu kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) imefanya ziara rasmi katika makao makuu ya muda ya Tanzania Bloggers Network (TBN) yaliyoipo Dar es salaam, Kijitonyama na kufanya mazungumzo ya kimkakati na viongozi wakuu wa mtandao huo.

Mazungumzo hayo yaliyolenga kujenga ushirikiano wa manufaa ya pande zote mbili yamejikita katika kuimarisha uhusiano wa kisekta kwenye masuala ya habari, uelimishaji wa umma, na usambazaji wa maarifa sahihi kuhusu mifumo ya pensheni na uwekezaji nchini.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, alieleza utayari wa mtandao huo kusimama kidete kama chombo cha kutoa elimu na kusambaza maarifa sahihi kwa umma na katika nyanja za kidijitali (space). Hata hivyo, alisisitiza kuwa ili kufikia malengo hayo kwa ufanisi zaidi, ni muhimu wanachama wa TBN wenyewe wakapatiwa kwanza mafunzo ya kina na ya kutosha kuhusu shughuli na uendeshaji wa mfuko huo.

Ushirikiano huo unatazamiwa kufungua ukurasa mpya katika matumizi ya vyombo vya habari vya mtandaoni kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi wengi zaidi nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa msafara huo kutoka PSSSF, Abdul Njaidi, alieleza kuwa ziara hiyo inalenga kujenga uhusiano wa karibu na wadau wa sekta ya habari pamoja na kutoa elimu kwa jamii. Aliwahakikishia viongozi wa TBN kuwa maombi na hoja zote zilizowasilishwa zitafanyiwa kazi, akisisitiza kuwa ushirikiano huo mpya unalenga kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mpana na sahihi kuhusu masuala ya pensheni na uwekezaji unaofanywa na PSSSF.

Naye Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi, ambaye alishiriki katika mkutano huo, alieleza kuwa mtandao huo wenye historia kubwa unajivunia weledi na ufanisi mkubwa.

Alisema TBN ipo kwa ajili ya kuhakikisha Tanzania inasomeka vyema katika medani za kidijitali ili kuchochea na kutanua zaidi gurudumu la maendeleo ya taifa.

Katibu wa TBN, Rahel Pallangyo, aliongeza kuwa mtandao huo upo tayari kutoa waandishi wake mahiri na kutumia majukwaa yake mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na za kuaminika zitakazowezesha kufanikiwa kwa utekelezaji wa majukumu ya wananchi na wadau wa maendeleo.

Katika mkutano huo, ujumbe wa PSSSF ulioongozwa na Abdul Njaidi, ulijumuisha maofisa wengine akiwemo Regina Kumba, Grayson Mgunda, na Doreen Lyimo.

Kwa upande wa TBN, viongozi waliohudhuria ni pamoja na Mwenyekiti Beda Msimbe, Katibu Rahel Pallangyo, mtaalamu wa mawasiliano, Cathbert Kajuna na Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi.










No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad