JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


PSPTB YAWAWEKEA MASHARTI WATAALAMU WENYE MADENI: WAPEWA SIKU 30 AU USAJILI WAO KUFUTWA

Share This


Na Janeth Raphael - MichuziTv

Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imewataka wataalamu wote waliosajiliwa ambao hawajalipa ada zao za mwaka kukamilisha malipo ya madeni yote ndani ya siku 30, ikionya kuwa watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo wanaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria, ikiwemo kufutiwa usajili na majina yao kuchapishwa rasmi.

Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Godfred Mbanyi, ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa wajibu wa wataalamu waliosajiliwa na Bodi. Amesema hatua hizo zinalenga kuhakikisha wataalamu wanatimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamia taaluma ya ununuzi na ugavi nchini.

PSPTB ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Fedha, iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi, Sura ya 179 ya Sheria za Tanzania. Bodi ina jukumu la kusimamia na kudhibiti viwango, mwenendo na maadili ya taaluma hiyo, huku ikiwa na mamlaka ya kusajili watu wanaokidhi vigezo na kuwapa uhalali wa kufanya kazi za kitaaluma katika eneo hilo.

Bodi imekumbusha kuwa ulipaji wa ada ya mwaka ni wajibu wa kisheria kwa kila mtaalamu aliyesajiliwa, kwa mujibu wa kanuni zake, ikiwemo Tangazo la Serikali Na. 364 la mwaka 2009. Mtaalamu anayeshindwa kulipa ada hiyo kwa kipindi cha miezi 24 mfululizo anaweza kupoteza hadhi ya usajili na jina lake kuondolewa kwenye daftari rasmi la PSPTB.

Aidha, PSPTB imeonya kuwa mtu anayeendelea kufanya kazi, kujitambulisha au kujihusisha na taaluma ya ununuzi na ugavi bila kuwa amesajiliwa na Bodi anafanya kosa la jinai na anaweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Kwa mujibu wa Kifungu cha 46(2) na (3) cha Sheria ya PSPTB, Bodi ina mamlaka ya kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu dhidi ya wanaokiuka masharti hayo.

Kwa hatua hiyo, PSPTB imewataka wataalamu wote wenye madeni ya ada ya mwaka kuhakikisha wamelipa madeni yao yote ndani ya siku 30 kuanzia tarehe ya tangazo hilo. Bodi imesisitiza kuwa watakaokaidi watachukuliwa hatua, ikiwemo kufutiwa usajili, kuchapishwa kwa majina yao na, pale inapobidi, kufunguliwa mashitaka kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha Bodi.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad