Na Mwandishi Wetu, Lindi
WATU wenye mahitaji maalum mkoani Lindi wametakiwa kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotokana na utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ikiwemo sekta ya mafuta na gesi asilia.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Lindi, Alusaria Mushi, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Adam Malima, wakati akifungua kongamano la siku moja la ushirikishwaji wa wazawa jumuishi.
Kongamano hilo limeandaliwa na Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na Sauti ya Wanawake Wenye Ulemavu Tanzania (SWAUTA).
Mushi amesema makundi hayo hayapaswi kujiona yameachwa nyuma, bali yanapaswa kutambua nafasi ya Kanda ya Kusini katika kuchangia ukuaji wa uchumi na kutumia fursa zinazotokana na miradi mbalimbali inayotekelezwa katika eneo hilo.
Amesema awali miradi ya Serikali ilikuwa ikibainisha mahitaji ya wananchi na kuyafanyia kazi, lakini kwa sasa wananchi wana wajibu wa kuibua mahitaji yao ili Serikali iweze kuhakikisha makundi yote yanahudumiwa kwa usawa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau kutoka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Charles Nyangi, amesema mamlaka hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali, wakiwemo watu wenye mahitaji maalum, wanawake, vijana na wazee.
Amesema lengo ni kuhakikisha makundi hayo yanapata fursa ya kushiriki na kunufaika na miradi ya mafuta na gesi asilia nchini.
“Katika utekelezaji wa miradi, kila mtu ana nafasi yake ya kushiriki na kunufaika. Hata kama kuna wawekezaji kutoka nje, wazawa wana nafasi ya kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na miradi hiyo,” amesema Nyangi.
Aidha, ameyataka makundi hayo kuwa na biashara zilizosajiliwa ili yaweze kushiriki katika fursa zitakapotangazwa katika maeneo yanayotekelezwa miradi, hususan mkoani Lindi.
Kongamano hilo la siku moja lilikuwa sehemu ya maandalizi kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Viziwi, ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Kilimanjaro.
Katika kuunga mkono maadhimisho hayo, PURA imegharamia ushiriki wa watu watano kutoka CHAVITA Wilaya ya Kibiti pamoja na kugharamia vifaa vya kusaidia usikivu.




No comments:
Post a Comment