Na Mwandishi Wetu
CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM), kupitia Mradi wa SAFARI unaotekelezwa kwa ushirikiano na Liverpool School of Tropical Medicine, kimebuni teknolojia ya matumizi ya akili Unde (Artificial Intelligence) inayolenga kusogeza huduma za uchunguzi wa ujauzito (Ultrasound) karibu na wajawazito wanaoishi katika maeneo yenye upungufu wa wataalamu wa afya.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, mtafiti wa mradi huo, Hamim Rushoke, amesema mfumo huo unatumia kifaa chenye Kumputa na probe maalumu inayowekwa tumboni kwa mjamzito, ambapo akili unde huchambua taarifa na kutoa majibu ndani ya dakika moja bila kuhitaji mtaalamu wa Ultrasound.
Amesema kifaa hicho kina uwezo wa kubaini umri wa ujauzito, hali ya uhai wa mtoto, mapigo ya moyo, idadi ya watoto waliopo tumboni pamoja na mkao wa mtoto ikiwa ametanguliza kichwa au miguu, kisha kutoa ripoti ambayo inaweza kusomwa na mhudumu yeyote wa afya.
"Teknolojia hii imebuniwa kuondoa changamoto ya ukosefu wa wataalamu wa ultrasound katika zahanati na vituo vya afya. Hata nesi au mkunga akipewa mafunzo ya siku mbili hadi tatu anaweza kuitumia kwa urahisi na kupata majibu sahihi kwa muda mfupi," amesema Rushoke. Ameeleza kuwa lengo kuu la mradi huo ni kuhakikisha wajawazito wa maeneo ya vijijini wanapata huduma za uchunguzi mapema, akibainisha kuwa wanawake wengi hufikia hatua ya kujifungua bila kufanyiwa hata kipimo kimoja cha ultrasound, jambo linaloweza kuhatarisha afya ya mama na mtoto. Kwa mujibu wa Rushoke, kwa sasa mradi huo uko katika hatua ya upembuzi yakinifu ukifanyika chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais-TAMISEMI, huku ukishirikisha viongozi wa afya, wajawazito na jamii ili kupima namna ambavyo ubunifu huo unapokelewa kabla ya kuidhinishwa kutumika nchini. "Tumepata ushirikiano mkubwa kutoka Wizara ya Afya, TAMISEMI, viongozi wa afya ngazi zote, wahudumu wa afya pamoja na wanawake wajawazito. Dalili zinaonyesha kuwa jamii ipo tayari kuupokea mfumo huu mara baada ya kukamilika kwa utafiti," amesema.
Aidha, amesema mradi huo umezingatia matumizi ya vifaa vya gharama nafuu ikilinganishwa na mashine za kawaida za ultrasound ambazo zinaweza kugharimu zaidi ya Sh milioni 80, wakati mfumo huo unahitaji tablet na probe zenye gharama zisizozidi Sh milioni tano kwa kifaa kizima.
Rushoke amesema mradi huo utaacha vifaa 32 katika zahanati na vituo vya afya 32 vya mkoa wa Dodoma vilivyotumika katika utafiti ili viendelee kutoa huduma bure kwa wananchi, huku akieleza kuwa hatua inayofuata ni Serikali kupanga bajeti ya kusambaza teknolojia hiyo katika maeneo mengine nchin




No comments:
Post a Comment