JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


VI Agroforestry yaandaa kongamano la vijana la kilimo misitu, washiriki 8,000 kutarajiwa Mara

Share This

 



Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SHIRIKA la VI Agroforestry linatarajia kufanya kongamano kubwa la vijana kuhusu kilimo misitu litakalofanyika mkoani Mara mwezi Oktoba mwaka huu, likiwa na lengo la kuwakutanisha zaidi ya washiriki 8,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza katika kongamano la wadau wa kilimo lililofanyika kwenye Maonesho ya Nane Nane katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkazi wa VI Agroforestry, Martha Olotu, alisema kongamano hilo linalenga kuwajengea vijana uelewa kuhusu fursa zilizopo katika kilimo misitu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Vijana, Joel Nanauka, ambaye atazungumza na vijana kuhusu nafasi yao katika sekta hiyo.

Olotu alisema VI Agroforestry imekuwa ikifanya kazi nchini kwa miaka 30, ikianzia mkoani Mara kabla ya kupanua shughuli zake katika mikoa ya Dodoma, Manyara, Lindi, Mtwara na Kagera. Aliongeza kuwa hadi sasa washiriki zaidi ya 3,000 tayari wamejisajili, huku lengo likiwa kufikia washiriki 8,000, kutoka 6,000 walioshiriki mwaka jana.

Alisema shirika hilo pia linakusudia kuanzisha mtandao wa mashirika yanayojihusisha na kilimo misitu ili kuimarisha ushirikiano na kuendeleza sekta hiyo.

Kwa upande wake, Edna Paul kutoka Counsenult alisema kilimo misitu kina mchango mkubwa katika kuhifadhi mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuongeza rutuba ya udongo na kuimarisha usalama wa chakula, hivyo kusaidia kupunguza utapiamlo.

Naye Mkurugenzi wa Civil Social Protective Foundation, Nemesi Kiliya, alisema wadau wanatarajia kuzindua jukwaa la wadau wa kilimo misitu litakalounganisha taasisi mbalimbali kushirikiana katika kukuza sekta hiyo.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad