Afisa Uratibu wa Ukuzaji Mitaala wa VETA Mhandisi Audiface Tarimo akizungumza na waandishi wa habari katika Banda la VETA kwenye Wiki ya Kitaifa ya Elimu,Ujuzi na Ubunifu linalofanyika Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga.
Na Mwandishi Wetu, Tanga
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) inatarajia kuzalisha wataalamu wazawa wapatao 400 katika sekta ya madini baada ya wataalamu wake kwenda nje ya nchi kupata mafunzo na kurejea nchini kwa ajili ya kuwajengea uwezo Watanzania.
Hatua hiyo inalenga kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi wa kisasa katika sekta ya madini, ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika miradi ya madini na kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi.
Akizungumza katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, Afisa Uratibu wa Ukuzaji Mitaala wa VETA, Mhandisi Audiface Tarimo, amesema mamlaka hiyo imezindua mitaala sita ya mafunzo ya uchimbaji wa madini chini ya ardhi kwa ajili ya watanzania kunufaika na rasilimali ya madini.
Tarimo amesema mitaala hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya soko la ajira na matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta ya madini.
Amesema sekta ya madini ni mhimili muhimu wa ukuaji wa uchumi kutokana na mchango wake katika uzalishaji, ajira, mapato ya Serikali na maendeleo ya viwanda, hivyo kuna umuhimu wa kuwa na nguvu kazi yenye ujuzi na weledi unaoendana na mabadiliko ya teknolojia.
“Wataalamu wetu wamekwenda nje ya nchi kujifunza na sasa wamerudi nchini. Kupitia ujuzi huo, tunatarajia kuzalisha Watanzania wapatao 400 watakaokuwa na uwezo wa kufanya kazi katika sekta ya madini,” amesema Tarimo.
Tarimo amesema utekelezaji wa mitaala hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha Watanzania wanapata nafasi kubwa zaidi katika sekta ya madini kwa kuwa na wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
Amesema hatua hiyo pia inaendana na utekelezaji wa sera ya ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini na inalenga kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi.
Mitaala hiyo inahusisha mafunzo ya Uendeshaji wa Mitambo ya Kubeba na Kusafirisha Miamba Migodini; Uendeshaji wa Mitambo ya Kuchimba Mahandaki; Uendeshaji wa Mitambo ya Kuchimba Mashimo Marefu, Uendeshaji wa Mitambo ya Kuchimba Mashimo ya Ndani ya Miamba; Maandalizi ya Ulipuaji wa Miamba Chini ya Ardhi,pamoja na Matumizi Salama ya Vifaa vya Kunyanyua na Kufunga Mizigo.
Tarimo amesema mafunzo hayo yatasaidia kujenga nguvu kazi ya Watanzania yenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchimbaji wa madini na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
.jpeg)


No comments:
Post a Comment