DAR ES SALAAM:
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari, amesema hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kumpendekeza Deogratius Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kukubaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kisha kupitishwa na Bunge kabla ya Septemba 4, 2026, haina changamoto yoyote ya kikatiba wala kisheria.
Johari ametoa ufafanuzi huo Bungeni leo, Agosti 28, 2026, wakati akijibu hoja zilizokuwa zikiibuliwa kuhusu muda wa uteuzi huo, huku baadhi ya watu wakidai kuwa Rais alipaswa kusubiri hadi Septemba 4, 2026 kabla ya kumteua Makamu wa Rais mpya.
Hoja hiyo ilijengwa kwa kurejea barua ya aliyekuwa Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi, ambayo ilieleza kuwa kujiuzulu kwake kungeanza rasmi Septemba 4, 2026, baada ya Rais kukubali ombi hilo.
Hata hivyo, Johari amesema wanaotoa hoja hiyo wamejikita zaidi katika Ibara ya 50(4) ya Katiba bila kuoanisha masharti yake na vifungu vingine, hususan Ibara ya 47 inayoweka masharti kuhusu mtu kushika nafasi ya Makamu wa Rais katika mazingira ambayo hayahusiani na uchaguzi mkuu.
Amesema tafsiri ya Ibara ya 50(4) haiwezi kufanywa kwa kuitazama ibara hiyo pekee, bali inapaswa kuhusishwa na vifungu vingine vya Katiba vinavyoweka masharti ya mtu kuwa na sifa au kupoteza sifa za kushika nafasi ya Makamu wa Rais.
Kwa mujibu wa Johari, miongoni mwa mazingira yanayoweza kusababisha mtu kupoteza sifa ya kushika nafasi hiyo ni pamoja na kupoteza uraia, kutiwa hatiani kwa makosa yanayotajwa na Katiba au kupoteza uanachama wa chama cha siasa.
Amesema katika mazingira ya Dkt. Nchimbi, baada ya CCM kumvua uanachama, tayari alishapoteza sifa ya kuendelea kushika nafasi ya Makamu wa Rais.
Kwa msingi huo, Johari amesema nafasi hiyo ilionekana kuwa wazi, hivyo kumpa Rais mamlaka ya kutumia Ibara ya 50(4) ya Katiba kumteua mtu mwingine bila kusubiri hadi Septemba 4, 2026.
“Suala la kujaza nafasi iliyo wazi ni tofauti na mchakato wa kumchagua Rais na Makamu wa Rais kupitia uchaguzi mkuu,” amesema Johari, akieleza kuwa Katiba imeweka utaratibu maalumu wa kushughulikia nafasi ya Makamu wa Rais inapokuwa wazi.
Amesema utaratibu huo unampa Rais mamlaka ya kupendekeza mtu wa kushika nafasi hiyo, huku uteuzi huo ukiwasilishwa Bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa kwa mujibu wa Katiba.
Mwanasheria Mkuu amewataka wanasheria na wananchi wanaojadili masuala ya kikatiba kuzingatia Katiba kwa ujumla wake wakati wa kutoa tafsiri ya vifungu vyake, badala ya kutumia ibara moja pekee kujenga hoja ya kisheria.
Amesisitiza kuwa vifungu vya Katiba vinapaswa kusomwa na kutafsiriwa kwa kuzingatia uhusiano wake na vifungu vingine, hasa pale vinapohusu sifa, madaraka na namna ya kujaza nafasi za viongozi wa kitaifa.
Ufafanuzi huo umeondoa hoja zilizokuwa zimeibuliwa kuhusu uhalali wa muda ambao Rais Samia alimpendekeza Ndejembi kushika nafasi ya Makamu wa Rais kabla ya tarehe Septemba 4, 2026.



No comments:
Post a Comment