Dar es Salaam, Agosti 31, 2026 Serikali ya Somalia imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha mageuzi ya utumishi wa umma kwa kujipanga kuanzisha Chuo cha Taifa cha Utumishi wa Umma huku ikilenga kutumia uzoefu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) katika uendeshaji wa taasisi ya mafunzo ya watumishi wa umma.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Shirikizo ya Somalia, Mhe. Hirsi Jama Ganni ulipotembelea Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) akiongoza ujumbe wa serikali hiyo ikiwa ni sehemu ya ziara rasmi ya siku nne nchini Tanzania iliyolenga kujifunza uzoefu wa Tanzania katika mageuzi ya sekta ya umma, mabadiliko ya kidijitali na maboresho ya mifumo ya Serikali.
Mhe. Ganni amesema Somalia imeweka mageuzi ya utawala wa umma kuwa moja ya vipaumbele vya kitaifa na kwamba mafanikio ya Serikali yanategemea kuwa na watumishi wenye ujuzi na uwezo wa kubadilisha sera na mipango kuwa matokeo halisi kwa wananchi.
“Somalia inapanga kuanzisha Chuo cha Taifa cha Utumishi wa Umma kitakachokuwa na jukumu la kutoa mafunzo kwa watumishi wa Serikali, kuanzia mafunzo ya awali kwa watumishi wapya hadi mafunzo kwa viongozi waandamizi. amesema Mhe. Ganni”
Mhe. Ganni ameongeza kuwa Tanzania imejenga mfumo ambao Somalia kwa sasa inalenga kuuanzisha, hivyo ziara hiyo imekuwa muhimu kwao katika kujifunza namna TPSC inavyoandaliwa, jinsi mitaala inavyotengenezwa na kusasishwa, pamoja na namna taasisi inavyoweza kuendelea kuwa na umuhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya vipaumbele vya Serikali.
“Tuna matumaini ziara hii itakuwa mwanzo wa ushirikiano wa muda mrefu katika maeneo ya uandaaji wa mitaala, kubadilishana wakufunzi na uzoefu, ujenzi wa taasisi pamoja na matumizi ya majukwaa ya kidijitali katika mafunzo,” amesema Mhe. Ganni
Dkt. Mabonesho amesema Somalia ilikuwa na chuo cha utumishi wa umma hapo awali, lakini taasisi hiyo ilishindwa kuendelea kufanya kazi kutokana na changamoto zilizotokana na vita, hivyo sasa nchi hiyo inapanga kuanzisha upya taasisi hiyo kwa kujifunza kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.
Ameeleza kuwa mafunzo ya utumishi wa umma ni muhimu kwa kuwaunganisha wataalamu kutoka kada mbalimbali wanaohudumu katika Serikali, wakiwemo madaktari, wahandisi na wahasibu, ili wote wawe na uelewa wa maadili, wajibu na namna bora ya kuwahudumia wananchi kwa heshima na staha.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mabonesho amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa pia kwa TPSC kutokana na uzoefu na maswali yanayotolewa na wageni hao, ambayo yanaweza kusaidia Chuo kutafakari na kuboresha baadhi ya maeneo ya utendaji.


No comments:
Post a Comment