Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imesema ushiriki wake katika Maonesho ya Nanenane 2026 unalenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya dawa za mifugo, taratibu za udhibiti wa bidhaa za dawa na vifaa tiba, pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kutengeneza dawa za mifugo nchini.
Akizungumza katika mahojiano maalum yaliyofanyika kwenye banda la TMDA katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea kitaifa jijini Dodoma, Meneja wa TMDA Kanda ya Kati, Sonia Mkumbwa, amesema mamlaka hiyo imeona ni muhimu kushiriki maonesho hayo ili kuwafikia wadau wa sekta ya kilimo na mifugo pamoja na wananchi kwa ujumla.
Amesema TMDA ina jukumu la kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa dawa na vifaa tiba vinavyotumika kwa binadamu na mifugo, hivyo maonesho hayo ni fursa muhimu ya kutoa elimu kuhusu huduma na majukumu ya mamlaka hiyo.
“Moja ya majukumu yetu makubwa ni kutoa elimu kwa umma. Tunatumia maonesho haya kuwaeleza wananchi matumizi sahihi ya dawa za mifugo, pamoja na kushirikiana na taasisi nyingine za umma, sekta binafsi na wajasiriamali katika kuimarisha huduma za afya ya mifugo,” amesema.
Mkumbwa ameeleza kuwa, TMDA ndiyo mamlaka yenye dhamana ya kusimamia uingizaji wa dawa za mifugo nchini, ambapo kila bidhaa inapaswa kusajiliwa na kupata kibali kabla ya kuingizwa nchini.
Amesema kabla ya usajili, mamlaka hufanya tathmini ya kina ili kuhakikisha bidhaa hizo zinakidhi viwango vya ubora, usalama na ufanisi, hatua inayolenga kulinda afya ya mifugo na watumiaji wa bidhaa zinazotokana na mifugo.
Aidha, amewataka wafugaji, wafanyabiashara na wadau wote wa sekta ya mifugo kuhakikisha wanatumia dawa zilizosajiliwa na kufuata taratibu zilizowekwa na TMDA.
Mbali na udhibiti wa dawa na vifaa tiba, Mkumbwa amesema TMDA inaendelea kuhamasisha wawekezaji kuanzisha viwanda vya kutengeneza dawa za mifugo na vifaa tiba nchini ili kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.
Amebainisha kuwa mamlaka hiyo ipo tayari kuwapa wawekezaji mwongozo na ushauri katika hatua zote za uanzishaji wa viwanda, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha uchumi wa viwanda na kuongeza thamani ya uzalishaji wa ndani.
Kwa upande wa huduma za uchunguzi wa maabara, Mkumbwa amesema TMDA ina maabara yenye ithibati ya Shirika la Afya Duniani (WHO), zinazofanya uchunguzi wa dawa za mifugo na vifaa tiba ili kuhakikisha bidhaa zinazotumika nchini zinakidhi viwango vinavyotakiwa.
Amesema huduma hizo zinapatikana katika makao makuu ya TMDA jijini Dodoma na katika maabara zake zilizopo Dar es Salaam.
Mkumbwa ametoa wito kwa wananchi, wafugaji na wawekezaji kutembelea banda la TMDA katika Maonesho ya Nanenane ili kupata elimu, ushauri na huduma mbalimbali zinazotolewa na mamlaka hiyo.
“Afya ya mifugo ni msingi wa usalama wa chakula na afya ya binadamu. Hivyo ni muhimu kuhakikisha bidhaa zote zinazotumika kutibu mifugo zinakuwa salama, bora na zenye ufanisi,” amesema.


.jpeg)
.jpeg)


No comments:
Post a Comment