Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) na Vodacom Tanzania PLC zimesaini makubaliano ya ushirikiano yenye lengo la kuharakisha mageuzi ya kidijitali katika mfumo wa uwekezaji nchini na kuboresha huduma kwa wawekezaji wa ndani na nje ya Tanzania.
Ushirikiano huo wa miaka miwili umewekwa rasmi kupitia Mkataba wa Makubaliano (MoU) uliosainiwa jijini Dar es Salaam jana, ukilenga kutumia teknolojia katika kurahisisha huduma za uwekezaji, kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuimarisha Tanzania kama eneo linalovutia uwekezaji endelevu na wenye thamani kubwa.
Kupitia makubaliano hayo, Vodacom Tanzania itatoa huduma mbalimbali za teknolojia kwa TISEZA, zikiwemo mawasiliano ya kibiashara, huduma za intaneti, teknolojia ya Internet of Things (IoT) pamoja na huduma za fixed internet.
Huduma hizo zinatarajiwa kusaidia TISEZA katika utekelezaji wa jukumu lake la kukuza, kuratibu na kuwezesha uwekezaji nchini, huku zikiboresha uzoefu wa wawekezaji katika hatua mbalimbali za uwekezaji.
Mbali na huduma za kiteknolojia, taasisi hizo zitashirikiana katika kuandaa shughuli za kutangaza fursa za uwekezaji nchini, ikiwemo mikutano ya wafanyabiashara, roadshows na majukwaa ya kuwafikia na kuwahudumia wawekezaji.
Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo leo Agosti 11, 2026, Mkurugenzi wa Biashara wa Vodacom Tanzania, Nguvu Kamando, amesema teknolojia imekuwa nyenzo muhimu katika kukuza uwekezaji, ubunifu na ushindani wa kiuchumi.
Amesema ushirikiano huo utaunganisha uwezo wa Vodacom katika teknolojia na jukumu la TISEZA la kukuza uwekezaji, kwa lengo la kujenga mazingira yaliyounganishwa zaidi, yenye ufanisi na rafiki kwa wawekezaji.
“Teknolojia imekuwa kichocheo muhimu cha uwekezaji, ubunifu na ushindani wa kiuchumi. Kupitia ushirikiano huu na TISEZA, tunaunganisha uwezo wa Vodacom katika teknolojia na dhamira ya Mamlaka ya kukuza uwekezaji,” amesema Kamando.
Amesema lengo ni kuhakikisha teknolojia inakuwa kichocheo cha uwekezaji kwa kuwezesha wafanyabiashara kupata mawasiliano na suluhisho za kidijitali zitakazowasaidia kuanzisha shughuli zao kwa haraka, kufanya kazi kwa ufanisi na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead J. Teri, amesema ushirikiano huo unaonyesha dhamira ya pamoja ya taasisi hizo katika kuboresha huduma kwa wawekezaji na kuendana na mwelekeo wa Tanzania wa kujenga uchumi unaotegemea ubunifu na teknolojia.
Amesema Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 inasisitiza umuhimu wa kuwa na uchumi wenye ushindani, unaoongozwa na ubunifu na unaoungwa mkono na miundombinu ya kisasa ya kidijitali pamoja na huduma bora za umma.
“Ushirikiano huu unaonyesha dhamira yetu ya pamoja ya kutumia teknolojia kuboresha uzoefu wa wawekezaji, kuimarisha uwezeshaji wa uwekezaji na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma,” amesema Teri.
Ameongeza kuwa kadiri Tanzania inavyoendelea kuvutia uwekezaji wa kimkakati katika sekta mbalimbali, ushirikiano na Vodacom utasaidia kuiweka nchi katika nafasi nzuri zaidi ya kuwa eneo linalopendelewa kwa uwekezaji endelevu na wenye thamani kubwa.
Ushirikiano huo pia unaendana na vipaumbele vya maendeleo ya taifa vya kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, pamoja na kutumia teknolojia za kidijitali kuboresha mfumo wa uwekezaji nchini.
Kupitia kuboresha mawasiliano, kuchochea ubunifu wa kidijitali na kuimarisha huduma zinazolenga wawekezaji, ushirikiano huo unatarajiwa kujenga mazingira ya uwekezaji yenye ufanisi, ushindani na yanayotumia teknolojia.
Vodacom Tanzania, ambayo ni miongoni mwa kampuni zinazoongoza katika teknolojia na mawasiliano nchini, imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali na suluhisho za kiteknolojia kwa ajili ya biashara, taasisi na jamii.
Ushirikiano huo na TISEZA unaelezwa kuwa sehemu ya jitihada za kampuni hiyo kuunga mkono ajenda ya Tanzania ya mageuzi ya kidijitali na kujenga mazingira yanayowezesha ubunifu, uwekezaji na ukuaji endelevu wa uchumi.










No comments:
Post a Comment