JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


TFRA YAWATAKA WAKULIMA KUJIANDAA MAPEMA KWA MSIMU WA KILIMO 2026/2027

Share This

 


Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MAMLAKA ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imesema Maonesho ya Kilimo na Mifugo ya Nane Nane ni fursa muhimu kwa wakulima kupata elimu na taarifa zitakazowasaidia kujiandaa kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2026/2027.

Akizungumza katika Maonesho ya Kilimo na Mifugo ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti Ubora wa TFRA, Happiness Mbelle, amesema wakulima wanapaswa kuhakikisha taarifa zao zimesajiliwa na kuhuishwa kwa wakati ili kuepuka changamoto wakati wa usambazaji wa mbolea.

Amesema mbolea inapatikana kwa kiasi cha kutosha, huku akiwataka wakulima kushirikiana na maafisa ugani katika kupima udongo ili kubaini mahitaji sahihi ya mbolea kulingana na aina ya mazao na hali ya udongo.

“Mkulima anapaswa kushirikiana na maafisa ugani kupima udongo ili kubaini mahitaji ya mbolea. Hii itasaidia kutumia mbolea kwa usahihi na kuongeza tija katika uzalishaji,” amesema Mbelle.

Aidha, amesema maonesho hayo ni fursa kwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini kupata elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, pamoja na huduma na majukumu ya TFRA.

Amesema TFRA itaendelea kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwawezesha kuelewa majukumu ya mamlaka hiyo na kuhakikisha wanapata huduma bora zenye viwango.

Mbelle amewataka wakulima kutumia fursa ya maonesho hayo kupata elimu na ushauri kutoka kwa wataalamu ili kuongeza ufanisi na tija katika shughuli za kilimo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad