JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Tanzania Yakamilisha Kwa Mafanikio Jukwaa la Miundombinu Afrika, Yaelekea Mkutano wa Wanahisa wa Africa50

Share This

 

Na Avila Kakingo
SERIKALI imesema Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum) limekamilika kwa mafanikio makubwa, huku sasa ikielekeza nguvu kwenye Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 unaofanyika leo Agosti 6, 2026.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema baada ya kukamilika kwa jukwaa hilo la siku mbili lililofunguliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wanahisa wa Africa50 wanakutana kujadili masuala ya uongozi na mwelekeo wa taasisi hiyo. Alisema yeye atakuwa mwenyekiti mwenza wa mkutano huo pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Sidy Ould Tah.

Waziri huyo amesema jukwaa hilo limewakutanisha viongozi wa serikali, taasisi za fedha za maendeleo, wawekezaji wa sekta binafsi na wadau wa kimataifa kujadili namna ya kuziba pengo la miundombinu barani Afrika na kuimarisha ushirikiano katika kugharamia miradi ya maendeleo. Aliongeza kuwa mjadala wa mwisho ulijikita katika mustakabali wa ushirikiano wa kimataifa (multilateralism), ambapo ilisisitizwa kuwa Afrika inapaswa kuongeza uwezo wa kujitegemea katika kufadhili na kutekeleza miradi yake ya maendeleo.

Aidha, amesema Tanzania imenufaika na mkutano huo kwa kusaini makubaliano matatu muhimu. Makubaliano hayo yanahusu ushirikiano kati ya TANESCO na Africa50 katika miradi ya usafirishaji wa umeme (transmission), mradi wa Mini LNG kati ya TPDC, Taqa Arabia na Africa50 kwa ajili ya kuchakata gesi asilia na kuiwezesha kutumika zaidi katika viwanda vya ndani, pamoja na makubaliano ya ujenzi wa kituo kipya cha huduma za usafishaji wa figo (dialysis) ili kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza nchini.

Balozi Khamis amesema kukamilika kwa jukwaa hilo na kutiwa saini kwa makubaliano hayo kunaonesha dhamira ya Tanzania ya kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuimarisha miundombinu, sekta ya nishati na huduma za afya kwa manufaa ya wananchi na ukuaji wa uchumi.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad