JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


HASARA YA SH. MILIONI 971.9 YAMPELEKA KAGALE JELA MIAKA 20

Share This

 



Na Mwandishi Wetu
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, imemhukumu mfanyabiashara Frank Kagale kifungo cha miaka 20 jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kukwepa kodi na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh milioni 971.9.

Aidha, mafundi wa mashine za kielektroniki EFD, Awadhi Mhavile (28), Ally Msesya (30), maarufu Ally Yanga, na Msimamizi wa Gereji, Salma Ndauka (26), wameachiwa huru baada ya Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.

Hukumu hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Is-haq Kuppa, baada ya kupitia ushahidi, utetezi, vielelezo pamoja na sheria zilinazohusiana na mashtaka hayo.

Hakimu Kuppa alisema Kagale ametiwa hatiani kwa makosa matatu likiwamo la kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara, kukwepa kulipa kodi na kudanganya mfumo wa kielektroniki.

"Kosa la kusababisha hasara, sheria inaelekeza adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 20 na kisichozidi miaka 30, huku kosa la kukwepa kulipa kodi likiwa na adhabu ya kulipa mara mbili ya kiasi cha kodi kinachodaiwa au kifungo cha miaka mitatu,"alisema Hakimu Kuppa

Kuhusu kosa la kusababisha hasara, alisema Mahakama imemtia hatiani na inakuhukumu kutumikia kifungo cha miaka 20 na kwa kosa la kukwepa kulipa kodi, adhabu yake ni kulipa mara mbili ya kiasi kinachodaiwa au kutumikia kifungo cha miaka mitatu.

"Kutokana na makosa haya kuhusiana kwa karibu, adhabu hizo zitatumikia kwa pamoja, hivyo Kagale atatumikia kifungo cha miaka 20 jela,"alisema Hakimu Kuppa

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Dickson Swai, aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa kutokana na ukubwa wa hasara iliyosababishwa kwa Serikali.

Swai alisema Serikali imepata hasara ya Sh. 971,977,771.32, fedha ambazo zilipaswa kutumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo kupitia ukusanyaji wa mapato ya ndani.

“Mheshimiwa, nchi imepata hasara ya Sh .971,977,771.32. Fedha hii imeleta pigo kwa uchumi wa Taifa kwa sababu Serikali inategemea ukusanyaji wa kodi ambao fedha hizo zilipaswa kuingia katika miradi mbalimbali nchini,” alidai Wakili Swai

Pia, alisema kosa hilo lina athari kwa uchumi wa nchi, hasa kutokana na umuhimu wa TRA katika ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Swai aliiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa Kagale na jamii kwa ujumla, akisisitiza kuwa kutokuwa na historia ya makosa ya jinai hakumaanishi mshtakiwa asipewe adhabu inayostahili kutokana na uzito wa makosa aliyotiwa hatiani.

Kwa upande wa utetezi, waliomba mahakama impunguzie Kagale adhabu kwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, kijana na tegemezi la familia na kwamba mahakama izingatie mazingira yake wakati wa kutoa adhabu.

Naye mshtakiwa Kagale alipopewa nafasi na Mahakama, aliiomba mahakama impunguzie adhabu, kwa sababu hajawahi kufanya kosa la jinai, analijutia kosa hilo na pia ana familia inayomtegemea, wakiwamo wazazi wake wazee, mke na watoto wadogo.

Pia aliiomba mahakama izingatie hali yake ya kiafya, akieleza kuwa anasumbuliwa na pumu na kwamba awali aliwasilisha cheti cha matibabu mahakamani na pia

Mahakama izingatie muda aliokaa mahabusu, akisema amekuwa mahabusu kwa takribani miaka mitatu.

Hata hivyo, Hakimu Kuppa alisema mahakama imezingatia uzito wa makosa, mazingira ya tukio pamoja na hoja zilizowasilishwa na pande zote kabla ya kutoa adhabu hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria.

Awali, upande wa mashtaka ulidai kuwa kati ya Mei 17 na Julai mwaka juzi, washtakiwa walitumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD) zilizozuiwa, kutoa risiti zisizo halali na kuisababishia TRA hasara.

Katika shtaka jingine, ilidaiwa kuwa kati ya Mei na Julai mwaka jana, washitakiwa walitumia mashine hizo kumdanganya Kamishna wa Kodi na kuwawezesha baadhi ya walipakodi kunufaika kwa njia isiyo halali, jambo lililosababisha TRA kupata hasara ya Sh 971,977,771.

Shauri hilo liliendeshwa na mawakili wa Serikali John Mwakifuna na Dickson Swai, huku TRA ikiwasilishwa na mawakili Auni Chilamula na Medalakini Emmanuel.

Baada ya hukumu, Wakili Chilamula aliwataka wananchi kuzingatia sheria za kodi, akiwataka wafanyabiashara kutoa risiti halali na wananchi kuchukua risiti halali wanapofanya manunuzi.

Alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha mapato ya ndani yanaendelea kukusanywa kwa ajili ya kuendesha shughuli za Serikali na kujenga Taifa linalojitegemea

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad