JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


GST YAZIDI KUIMARISHA HUDUMA ZA MAABARA, YALENGA KUONGEZA TIJA KWA WACHIMBAJI NA WAWEKEZAJI

Share This

 



Dodoma
TAASISI ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeeleza kuwa inaendelea kuimarisha huduma zake za maabara kwa kutoa uchunguzi wa sampuli mbalimbali za madini, tafiti za uchenjuaji pamoja na ushauri wa kitaalamu unaolenga kuongeza tija katika shughuli za uchimbaji na uwekezaji katika sekta ya madini.

Akizungumza kuhusu huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Maabara wa GST, Bw. Notka Banteze, amesema GST ina uzoefu mkubwa katika utoaji wa huduma za maabara, huku maabara yake ikiwa imetimiza miaka 100 katika kuhudumia sekta ya madini nchini.

Amesema kupitia maabara hizo, GST hufanya uchunguzi wa sampuli mbalimbali za madini na kutoa majibu yanayomsaidia mdau kufanya maamuzi sahihi kuhusu shughuli za uchimbaji, uchenjuaji na uwekezaji.

“Tunatoa uhakika kwa wawekezaji kwa kuwapatia majibu yanayoaminika kupitia maabara zetu zenye ithibati. Huduma hizi zinamwezesha mdau kupata taarifa sahihi za kisayansi kabla ya kufanya maamuzi katika shughuli zake za madini,” amesema Banteze.

Amesema mbali na uchunguzi wa sampuli, GST pia inafanya tafiti za uchenjuaji wa madini kwa lengo la kumsaidia mchimbaji kutumia njia sahihi za uchimbaji na uchenjuaji ili kuongeza kiwango cha madini anachopata na kupunguza upotevu wa madini.

“Wachimbaji wengi wamekuwa wakipoteza madini mengi yaliyopo kwenye miamba kutokana na kutofanya tafiti bora za uchenjuaji. Sisi tunafanya tafiti hizo maabara na pia tunawafikia wachimbaji katika maeneo yao ya kazi ili kuwapatia ushauri wa kitaalamu kuhusu namna bora ya kuchimba na kuchakata madini kulingana na aina ya madini wanayochimba,” amesema.

Ameongeza kuwa GST pia imejikita katika uzalishaji wa bidhaa zinazotumika katika uchunguzi wa sampuli za madini, ikiwemo vyungu vya kuyeyushia sampuli za dhahabu (crucibles) pamoja na vyungu vidogo vinavyotumika katika uchunguzi wa sampuli mbalimbali za dhahabu.

Amesema bidhaa hizo zinazalishwa kwa ukubwa wa aina nne ambazo ni D30, D40, D50, na D55 zinaweza kutumiwa na wadau mbalimbali, wakiwemo wanaoendesha maabara za uchunguzi wa madini.

Sambamba na hayo, amesema GST inaishukuru Serikali kwa kuendelea kuiwezesha Taasisi hiyo kuimarisha miundombinu ya huduma za maabara, ikiwemo ujenzi wa maabara kubwa na ya kisasa katika eneo la Kizota, Dodoma.Amesema maabara hiyo inalenga kuwa kituo muhimu cha huduma za uchunguzi wa sampuli za madini kwa Tanzania pamoja na nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Aidha, amesema GST inaendelea na ujenzi wa maabara ndogo za Kanda katika maeneo yenye shughuli kubwa za uchimbaji wa madini, ikiwemo Chunya na Geita, hatua inayolenga kusogeza huduma za maabara karibu zaidi na wachimbaji na wadau wengine wa sekta ya madini.

Amesema uwepo wa huduma hizi karibu na maeneo ya uchimbaji utasaidia wachimbaji kupata taarifa za kisayansi kwa wakati, kufanya maamuzi sahihi na hatimaye kuongeza ufanisi na tija katika uzalishaji wa madini nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad