Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB) Lwaga Mwambande akizungumza na Kundi la Wanawake waliotembelea Banda la DIB katika Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa Nane Nane yanayoendelea kwenye Viwanja vya Dkt.John Samwel Malecela Nzuguni Jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
BODI ya Bima ya Amana (DIB) imewataka wananchi kuhakikisha wanaweka na kuhifadhi fedha zao katika taasisi za fedha zilizosajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kulinda amana zao dhidi ya hasara zinazoweza kujitokeza.
Hayo ameyasema Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa DIB,
Lwaga Mwambande, wakati akizungumza na kundi la wanawake waliotembelea banda la DIB katika Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Mwambane amesema kuweka fedha katika taasisi za fedha zilizosajiliwa ni njia salama, kwani wananchi wanaweza kupata ulinzi wa amana zao hata endapo taasisi husika itafungwa kwa mujibu wa taratibu na sheria.
Amesema wananchi wanapaswa kuepuka tabia ya kuhifadhi fedha kwa njia zisizo rasmi, ikiwemo fedha za vikundi vya kijamii kushikiliwa na mtu mmoja au kuwekwa kwenye vikapu na vibubu, kwa kuwa njia hizo zinaweza kusababisha hasara iwapo fedha zitapotea.
“Usalama wa kuhifadhi Fedha ni benki ,Fedha zinapokuwa katika taasisi zilizosajiliwa zinakuwa salama, na hata benki ikifungwa, mwananchi hapotezi amana zake,” amesema Mwambane.
Amesema wananchi waliokuwa wameweka amana zao katika baadhi ya benki zilizofungwa wameweza kulipwa kwa mujibu wa utaratibu wa bima ya amana.
“Kuweka fedha katika taasisi zisizo rasmi kunaweza kuwanyima wananchi haki ya kupata fidia endapo taasisi hizo zitashindwa kutekeleza majukumu yake", amesema.
Aidha, Mwambane amewahimiza wananchi, hususan wanawake, kutumia fursa ya Maonesho ya Nane Nane kutembelea banda la DIB na kupata elimu kuhusu usalama wa amana, pamoja na umuhimu wa kuhifadhi fedha katika taasisi za fedha zilizosajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania.
.jpeg)
.jpeg)


No comments:
Post a Comment