JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Wanawake Bahi Wahimizwa Kuvunja Ukimya Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia

Share This

 



Na Mwandishi Wetu, Bahi

Wanawake wa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma wamehimizwa kupaza sauti dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoendelea kuathiri wanawake, watoto na maendeleo ya jamii.

Wito huo umetolewa katika mdahalo ulioandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), ukiwaleta pamoja wanawake na viongozi mbalimbali kujadili namna ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia.

Akifungua mdahalo huo, Mkurugenzi wa TAMWA, Dk. Rose Reuben amesema ukatili wa kijinsia una sura nyingi na huathiri watu kwa namna tofauti.

"Kuna ukatili wa aina nyingi na kila mmoja amepitia kwa aina yake. Tupo hapa kujifunza ili kupata maarifa zaidi na kwa pamoja tuendelee kupaza sauti zetu," alisema.

Afisa Elimu Mkoa wa Dodoma, Kumburusa Elias, alisema jamii bado inakabiliwa na changamoto ya kutokuchukua hatua dhidi ya vitendo vya ukatili, hata pale vinapotokea ndani ya familia.

"Ukatili wa wanawake upo na tunauona, lakini kwa bahati mbaya sisi wanawake wenyewe hatuchukui hatua kupaza sauti zetu. Utamkuta mama anaungana na baba kuhakikisha mtoto mlemavu haendi shule kwa kuogopa aibu," alisema.

Aliongeza kuwa baadhi ya watoto wa kike bado wananyimwa haki ya elimu kwa shinikizo la wazazi wanaotaka waolewe mapema.

"Usikubali mtoto wako wa kike akatishwe elimu na baba kwa kigezo cha kuolewa. Tafuta namna yoyote kwa siri utoe taarifa zitakazomsaidia kupata haki yake," alisisitiza.

Naye Afisa Maendeleo Mkoa wa Dodoma, Neema, aliwataka wanawake kutumia fursa za vikundi vya kiuchumi kujiondoa kwenye utegemezi unaochochea ukatili wa kiuchumi.

"Kama mradi wa TAMWA unavyosema Sauti Zetu, sisi wamama tupaze sauti zetu kwa pamoja kukemea ukatili wa aina zote. Tunalo jukumu la kutumia fursa za vikundi kujikwamua kiuchumi na kuwa mabalozi wa kupinga ukatili," alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake, Janeth Nyamayahasi, alisema baadhi ya vitendo vya ukatili vimezoeleka kiasi cha kutotambuliwa kama ukatili.

"Wakati mwingine sisi wenyewe tunafanya ukatili bila kujua. Tunao watoto wa kike wanaolazimishwa kwenda kufanya kazi mijini ili kusaidia familia, huku wanawake wakikosa haki ya kuamua matumizi ya mazao wanayoyalima. Huu pia ni ukatili," alisema.

Akizungumza kuhusu hatua za kisheria zinazopatikana kwa wahanga, Mrakibu wa Polisi kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Dodoma, Christa Yasinta Kayombo, alisema madawati hayo yameanzishwa katika vituo vya polisi ili kusaidia wahanga kwa usiri na weledi.

"Dawati la Jinsia na Watoto ni ofisi maalumu iliyoanzishwa katika kila kituo cha polisi. Tunafanya kazi kwa usiri na weledi kusaidia wahanga wa ukatili wa kijinsia. Jiamini kabisa unapotoa taarifa, itabaki kuwa siri," alisema.

Mrakibu Kayombo alisema ukatili ni kosa la kisheria na haukubaliki kwa misingi ya dini wala utu.

"Ukatili kwa imani zote ni dhambi, penye ukatili hakuna upendo. Vitendo vya ukatili vinakiuka sheria na vinapaswa kukemewa na kila mwanajamii," alisema.

Pia aliitaka jamii kuacha kuficha vitendo vya ukeketaji, ulawiti na aina nyingine za ukatili vinavyofanywa dhidi ya watoto wa kike na wa kiume.

Mdahalo huo umefanyika chini ya mradi wa Sauti Zetu unaotekelezwa na TAMWA kwa kushirikiana na GIZ, ukiwa na lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu haki za wanawake na watoto na kuhamasisha wananchi kushiriki katika kutokomeza ukatili wa kijinsia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad