Na Mwandishi Wetu
Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira (TRAMEPRO) limesema linasikitishwa kuhusu kuongezeka kwa vitendo vya utapeli wa mitandaoni vinavyotumia picha, majina, nembo na utambulisho wa viongozi wa Serikali na watu maarufu kwa lengo la kuwadanganya wananchi na kujipatia fedha kwa njia zisizo halali.
Limesema kumekuwepo na matangazo yanayodai kuwa viongozi mbalimbali, wafanyabiashara au taasisi zinatoa mikopo, ruzuku (grants), misaada au uwekezaji wa haraka na matangazo hayo huambatana na ushuhuda wa uongo ili kuwafanya wananchi waamini.
Akizungumza kuhusu utapeli wa mitandaoni Katibu Mkuu wa TRAMEPRO ambaye pia ni Mtaalam wa Tiba Asili Boniventura Mwalongo amesema shirika hilo linatoa tahadhari kwa wananchi wote kutokukubali kushawishiwa na matangazo hayo bila kuyathibitisha kupitia mamlaka au taasisi husika.
Amesisitiza wananchi wanapaswa kutumia taarifa zinazotolewa kupitia njia rasmi pekee na kuepuka kutuma fedha, nyaraka au taarifa binafsi kwa watu wasiojulikana.
“Tunasikitishwa na matumizi mabaya ya nembo na majina ya vyombo vya habari pamoja na viongozi wa kitaifa katika kusambaza taarifa za uongo. Vitendo hivyo vinachochea upotoshaji wa umma, huondoa imani kwa taasisi na vinaweza kuhatarisha usalama, amani na mshikamano wa Taifa.
“TRAMEPRO inaona bado kuna haja ya kuimarisha juhudi za kutokomeza mila potofu zinazodhuru afya, utu na haki za binadamu.Zipo taarifa na tafiti zinazoonyesha baadhi ya mila potofu zinaendelea kufanyika kwa siri katika maeneo mbalimbali. Hali hii inaonyesha kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado elimu, ufuatiliaji na ushirikiano wa wadau vinahitaji kuimarishwa zaidi.”
Amesema TRAMEPRO inatoa rai kwa Serikali kuimarisha mapambano dhidi ya utapeli wa mtandaoni kupitia vyombo vya dola na mamlaka zinazohusika.Kuendelea kutoa elimu ya matumizi salama ya mitandao ya kijamii na huduma za kidijitali.
Pia kufufua au kuimarisha mifumo ya kitaifa ya uratibu wa mapambano dhidi ya mila potofu kwa kushirikisha sekta zote muhimu pamoja na kuongeza uwekezaji katika tafiti, elimu ya afya na kampeni za mabadiliko ya tabia.
Wakati kwa mamlaka za mawasiliano na usalama zimeshauriwq kuchukua hatua za haraka dhidi ya akaunti na mitandao inayotumika kufanya utapeli na kusambaza taarifa za uongo.
Aidha kuongeza uwezo wa kufuatilia na kuwachukulia hatua wahalifu wa mtandaoni,kushirikiana na kampuni za mitandao ya kijamii kuondoa akaunti bandia zinazojifanya viongozi au taasisi.
Mwalongo pia ametoa rai kwa wananchi wasiamini matangazo yanayoahidi fedha, mikopo au ruzuku bila uthibitisho na kuwataka wathibitiahe taarifa kupitia ofisi au tovuti rasmi.
“TRAMEPRO inaamini jamii salama, yenye afya na maendeleo endelevu hujengwa kwa msingi wa ukweli, elimu, uwajibikaji na ushirikiano. Tunatoa wito kwa kila mwananchi kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya utapeli wa mtandaoni, taarifa za uongo na mila potofu zinazokwamisha maendeleo ya Taifa.”



No comments:
Post a Comment