JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Shirika la From Hearts 2 Hands lajenga maktaba kunufaisha wanafunzi 737 wa jamii ya Kimasai

Share This

 

Mkuu wa Wilaya ya Monduli , Gloriana Kimath akikata utepe kuzindua maktaba mpya iliyojegwa na Shirika la From Hearts 2 Hands kupitia mwanzilishi wake , Dkt Briana Greene (kulia kwa Mkuu wa Wilaya)  ambayo inafungua fursa ya  kujifunza , utamaduni wa kujisomea , kupanua maarifa na kuongeza ufaulu wanafunzi wa Shule ya Msingi Lendikinya ya jamii ya wafugaji wa kimasai wilayani Monduli mkoani Arusha.

Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la From Hearts 2 Hands kupitia mwanzilishi wake, Dkt. Briana Greene, limezindua maktaba itakayohudumia wanafunzi 737 wa Shule ya Msingi Lendikinya kutoka jamii ya wafugaji wa Kimasai wilayani Monduli. Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Gloriana Kimath, aliipongeza taasisi hiyo kwa kujenga maktaba ambayo ni miongoni mwa maktaba bora zaidi katika Mkoa wa Arusha, akisema ushirikiano kati ya Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali umeendelea kuleta matokeo chanya katika kuboresha huduma za jamii, hususan sekta ya elimu.

Kimath alisema anatamani wakuu wa wilaya nyingine wafike kuona maktaba hiyo na kujifunza, akieleza kuwa pamoja na uzuri wa jengo, jambo muhimu ni kuhakikisha linatumika ipasavyo kwa kujenga utamaduni wa watoto kujisomea vitabu. Alibainisha kuwa maktaba hiyo ina vitabu vya historia, sayansi, lugha na sanaa pamoja na vifaa vya kujifunzia vitakavyowawezesha watoto kukuza vipaji na ubunifu wao.

Pia aliwataka wazazi kuhakikisha watoto wanaendelea kujisomea hata wanaporejea nyumbani na kutowabagua watoto wa kike katika kupata elimu. Alisema mtoto wa kike ana uwezo wa kufikia nafasi mbalimbali za uongozi na kusisitiza kuwa wasikatizwe ndoto zao kwa ukeketaji, ndoa za utotoni au vitendo vingine vinavyowanyima haki ya elimu.

Aidha, aliwataka wananchi na viongozi wa kijiji kuilinda maktaba hiyo kwa kuwa ni mali ya jamii nzima, huku akihimiza kuendelea kuwekeza katika elimu. Alisema Monduli imeendelea kufanya vizuri kitaaluma, ikiongoza Mkoa wa Arusha katika matokeo ya Kidato cha Nne na kutokuwa na Daraja la Nne wala sifuri katika matokeo ya Kidato cha Sita.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Dkt. Briana Greene alisema uwekezaji katika elimu ni njia bora ya kubadilisha maisha ya watoto wa jamii ya wafugaji. Alieleza kuwa alianza kusaidia shule hiyo kwa kujenga tenki na miundombinu ya maji baada ya kubaini changamoto zilizokuwepo kabla ya kuendelea na ujenzi wa maktaba kupitia taasisi yake ya From Hearts 2 Hands, akisema watoto wa Lendikinya wanapaswa kupata fursa sawa na watoto wengine duniani.

Greene alisema aliona umuhimu wa wanafunzi kupata vitabu karibu ili kuwafungulia fursa ya kujifunza zaidi, akieleza kuwa baada ya kuona changamoto ya maji alijenga tenki, kisha akaona kuna haja ya kujenga maktaba. Alisema anatamani utamaduni wa Kimasai uendelee huku watoto wakipata maarifa mapya yatakayochochea maendeleo ya jamii yao.

Aliwataka wazazi wa jamii ya Kimasai kuwapeleka watoto wote shule, hususan wasichana, akisema elimu ndiyo njia ya kuvunja mzunguko wa umaskini na kuwawezesha watoto kujitegemea. Pia aliwaomba wanafunzi kuitunza maktaba hiyo na vifaa vyote vilivyomo kwa kuwa ni rasilimali yao muhimu.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi, Diwani wa Kata ya Sepeko, Joseph Kimaay, alisema ujenzi wa maktaba hiyo utasaidia kukuza na kuboresha elimu, akibainisha kuwa katika kata na wilaya hiyo hakuna maktaba nyingine kama hiyo na kwamba ushirikiano kati ya Serikali na wadau binafsi umewezesha kufanikisha mradi huo.

Akisoma risala, Mwalimu Mkuu Solomon Godfrey alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1977 ina wanafunzi 737, wakiwemo wavulana 331 na wasichana 406 pamoja na walimu wanane. Alisema maktaba hiyo imewekewa samani, vitabu vya aina mbalimbali, vifaa vya michezo, muziki, sanaa, kompyuta na maeneo ya watoto kujifunzia kwa vitendo, na kwamba itasaidia kuongeza utamaduni wa kujisomea, kuboresha mazingira ya ujifunzaji na kuongeza kiwango cha ufaulu kutoka asilimia 86.02 kilichofikiwa mwaka 2025. Aliongeza kuwa shirika hilo pia limejenga tanki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 100,000, kugawa matenki ya maji kwa wananchi, kujenga nyumba za kuvunia maji ya mvua na kugawa chupa 700 za kubebea maji kwa wanafunzi.

Naye mwanafunzi wa Darasa la Sita, Riziki Papaking, aliwashukuru wadau wa elimu kwa kufanikisha ujenzi wa maktaba hiyo, akisema itawapa wanafunzi mazingira bora ya kujisomea, kuongeza maarifa, kufanya vizuri katika masomo na kutimiza ndoto zao.
Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Gloriana Kimath (Kulia), akipata maelezo mbalimbali kuhusu Maktaba hiyo kutoka kwa mwanzilishi wa From Hearts

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad