Serikali kupitia Sheria ya Madini Kifungu cha 9 imepiga marufuku raia wa kigeni kumiliki leseni ndogo za uchimbaji wa madini.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wazawa wanafaidika na rasilimali za madini zilizopo katika ardhi yao.
Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde amesema hayo wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo Mkoa wa Geita, katika kata ya Igalula, Wilaya ya Nyang'hwale.
Amesema sheria hiyo inawalinda wazawa wanaohitaji maeneo ya kuchimba ili wanufaike na madini.
Hata hivyo Mavunde amefafanua kuwa kupitia Kifungu cha 3, raia wa kigeni anaweza kuingia katika leseni ndogo kama mshauri wa kiufundi wa mchimbaji mdogo.
Katika utaratibu huo mpya, mwenye leseni atapata asilimia 30 tofauti na awali iliyokuwa chini.
Aidha Waziri amemuelekeza Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini Mbogwe, Bw. Jeremia Hango kufuatilia leseni zote zisizofanyiwa utafiti kwa muda mrefu.
Amesema amefuta leseni 70 za utafiti mkubwa zikiwemo zile za Mkoa wa Kimadini Mbogwe, baada ya kubaini kuna maeneo yenye wamiliki lakini hayafanyiwi kazi.
Mavunde ameongeza kuwa leseni hizo zitagawiwa kwa Watanzania wote bila upendeleo wala kujuana na viongozi ili kila mmoja anufaike na rasilimali za madini.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella amesisitiza leseni "bubu" zifutwe mara moja ili wananchi wapate maeneo ya uchimbaji.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)



No comments:
Post a Comment