JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Serikali Yaimarisha Maandalizi Dhidi ya Ebola, Yaonya Kuhusu Upotoshaji wa taarifa

Share This

 

Na Mwandishi Wetu.
SERIKALI imeimarisha kwa kiwango kikubwa ufuatiliaji katika mipaka, vituo vya kuingilia nchini na mfumo mzima wa huduma za afya ili kuzuia ugonjwa wa Ebola kuingia nchini kutoka mataifa jirani.

Akizungumza katika semina ya wanahabari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi wa Ukuzaji wa Afya kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Rahma Hingora, alisema kuwa licha ya Tanzania kutokuwa na kisa chochote cha Ebola, ufuatiliaji umeimarishwa katika vituo vyote vya mipakani, viwanja vya ndege, bandari na vituo vikuu vya usafiri.

"Ingawa Tanzania haina mlipuko wa Ebola kwa sasa, hatuchukulii jambo hili kwa uzembe," alisema Dkt. Hingora.

"Tunaendelea kuimarisha maandalizi ya dharura, kuongeza uwezo wa wahudumu wa afya na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa ili kulinda taifa."
Dkt. Hingora alisisitiza kuwa utoaji wa taarifa sahihi na kwa wakati ni muhimu sawa na maandalizi ya kitabibu, akionya kuwa uvumi na taarifa potofu husababisha hofu, hupunguza imani ya wananchi kwa mamlaka za afya na kudhoofisha juhudi za kukabiliana na milipuko.

Aliwataka wanahabari kuripoti kwa uwajibikaji kwa kutumia taarifa zilizothibitishwa kutoka vyanzo rasmi, akieleza kuwa vyombo vya habari ni washirika muhimu katika kulinda afya ya umma.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mkuu wa Kitengo cha Mabadiliko ya Kijamii na Tabia wa UNICEF Tanzania, Dkt. Awete Araya, ambaye alikumbusha mafunzo yaliyopatikana kutokana na milipuko ya Ebola iliyowahi kutokea Afrika Magharibi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

"Silaha yenye nguvu zaidi katika maandalizi dhidi ya Ebola ni taarifa zinazoaminika," alisema Dkt. Araya mbele ya wanahabari na washawishi wa mitandao ya kijamii.

"Jamii huchukua hatua kulingana na kile wanachosikia, wanachoamini na wanachokiona kwenye mitandao ya kijamii. Ninyi si watazamaji tu, bali ni wahusika wa mstari wa mbele katika kukabiliana na dharura za afya."

Alionya kuwa taarifa za uongo zinaweza kuzifanya familia kuficha wagonjwa na kupoteza imani kwa mamlaka za afya, jambo linaloweza kuchelewesha hatua muhimu za kuokoa maisha.

Dkt. Araya alisema UNICEF itaendelea kuisaidia Tanzania katika mawasiliano ya hatari, ushirikishwaji wa jamii, udhibiti wa maambukizi pamoja na kuboresha huduma za maji, usafi na mazingira, huku watoto walio katika mazingira hatarishi wakiendelea kuwa kipaumbele katika mwitikio wa dharura.

Kwa upande wa utekelezaji, hatua za ulinzi tayari zimeanza kutekelezwa.
Ofisa Mkuu wa Afya wa Bandari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dkt. Mustapha Mpagama, alisema mamlaka zimeweka vifaa vya kisasa vya kupima joto la mwili katika maeneo ya kuingilia nchini na kutoa mafunzo maalumu kwa wahudumu wa afya wanaofanya kazi mipakani.

Aidha, alisema ongezeko la watu wanaovuka mipaka limeifanya Serikali kuimarisha zaidi hatua za kujikinga dhidi ya kuenea kwa ugonjwa huo.

Alieleza kuwa usafiri wa anga, barabara, usafirishaji wa mizigo na biashara za mipakani ni miongoni mwa njia zinazoweza kuchangia kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko ikiwa tahadhari hazitachukuliwa.

Washiriki wa semina walikubaliana kuoanisha njia za mawasiliano ili kuhakikisha kuwa tishio lolote la kiafya katika ukanda huu linakabiliwa kwa kutoa elimu ya haraka, sahihi na inayozingatia ukweli.

Kwa sasa Tanzania inaendelea kubaki huru dhidi ya Ebola bila kuwa na kisa chochote kilichothibitishwa nchini.

Hata hivyo, kutokana na milipuko inayoendelea katika nchi jirani kama Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha ufuatiliaji, uchunguzi wa wasafiri mipakani pamoja na hatua nyingine za kinga katika vituo vyote vya kuingilia nchini.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad