JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


SEMA NA WAZIRI YAAMSHA MATUMAINI; KERO 29 ZA WANANCHI ZAANZA KUPATIWA UFUMBUZI

Share This


Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kuimarisha huduma za upatikanaji wa haki kwa wananchi kupitia programu ya "Sema na Waziri", ambapo jumla ya malalamiko 29 yamepokelewa na kuanza kufanyiwa kazi, hatua inayotoa matumaini kwa wananchi wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za kisheria.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, leo Julai 14, 2026, alipokuwa akipokea simu na kusikiliza kero za wananchi katika ofisi za Wizara zilizopo Mtumba, jijini Dodoma.

Dkt. Homera amesema kipindi hicho kimeendelea kuwa daraja muhimu kati ya Serikali na wananchi, kwa kuwa kinawapa nafasi ya kuwasilisha malalamiko yao moja kwa moja kwa uongozi wa wizara ili yapatiwe ufumbuzi kwa mujibu wa sheria.

Amesema katika zoezi la leo, Wizara imepokea simu 29 zenye malalamiko yanayohusu masuala mbalimbali ya kisheria na kijamii, ambapo baadhi ya kesi zimeanza kushughulikiwa mara moja, huku nyingine zikipelekwa kwenye taasisi na mamlaka husika kwa hatua stahiki.

Akifafanua baadhi ya malalamiko yaliyopokelewa, Dkt. Homera amesema miongoni mwa waliojitokeza ni Ali Shabani Magome kutoka Dar es Salaam, aliyeripoti tukio la nyumba yake kuchomwa moto, pamoja na Salumu Abdala Namtuka, ambaye alidai kupigwa risasi kufuatia mgogoro wa ardhi. Aidha, Ahmed Kitwana kutoka Zanzibar na wananchi wengine kutoka maeneo mbalimbali nchini waliwasilisha kero zao ambazo zimepokelewa na kuanza kufanyiwa kazi kupitia mifumo ya utoaji haki.

Amesisitiza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kutumia jukwaa la "Sema na Waziri" kama sehemu ya kuwasikiliza wananchi, kufuatilia changamoto zao na kuhakikisha kila anayestahili haki anapata huduma kwa wakati na kwa kuzingatia misingi ya sheria.

Dkt. Homera amewahimiza wananchi kuendelea kutumia fursa hiyo kueleza changamoto zao kwa njia halali, akibainisha kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha huduma za kisheria zinawafikia wananchi kwa ufanisi, uwazi na haki.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad