JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


NSSF: Wananchi Waliojiajiri Jiungeni, Jiwekeeni Akiba kwa Kesho Yenye Uhakika

Share This


Dar es Salaam, Julai 10, 2026

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umewahimiza wananchi waliojiajiri nchini kujiunga na kuchangia katika Mfuko huo ili kujijengea akiba, kupata kinga ya kijamii na kuwa na uhakika wa maisha ya sasa na baadaye.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Ekwabi Mujungu, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, wakati akifungua Siku Maalumu ya Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi Waliojiajiri iliyofanyika Julai 10, 2026 katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Bw. Mujungu alisema Siku Maalumu ya Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi Waliojiajiri ni sehemu ya mkakati wa NSSF wa kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii kwa wananchi waliojiajiri, ambao ni sehemu muhimu ya ukuaji wa uchumi wa nchi.

"Wananchi wengi wanaojiajiri hupata kipato kupitia shughuli wanazozifanya, lakini bila kuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba wanaweza kujikuta wakikabiliwa na changamoto wanapofikia uzee au wanapopoteza uwezo wa kufanya kazi. Kujiunga na NSSF ni hatua muhimu ya kujenga uhakika wa maisha ya sasa na ya baadaye," alisema Bw. Mujungu.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya kupanua wigo wa hifadhi ya jamii ili wananchi wote, bila kujali aina ya shughuli wanazofanya, wanufaike na huduma za mifuko ya hifadhi ya jamii.

"Tunawahimiza wananchi wote waliojiajiri kutumia fursa hii kujiunga na kuchangia NSSF. Mtu anapoanza kuweka akiba mapema, anajijengea msingi imara wa kunufaika na mafao mbalimbali yatakayomsaidia yeye na familia yake pale yatakapohitajika," alisisitiza.

Kwa upande wake, Meneja wa NSSF Mkoa wa Kigamboni, Bw. Siraji Kisaka, alisema siku hiyo maalumu imeandaliwa mahsusi kuwafikia wananchi waliojiajiri kwa kuwapatia elimu kuhusu umuhimu wa kujiunga na kuchangia NSSF pamoja na kuwafahamisha mafao na huduma mbalimbali zinazotolewa na Mfuko.

"Lengo letu ni kuhakikisha wananchi waliojiajiri wanapata uelewa sahihi kuhusu hifadhi ya jamii na umuhimu wa kujiunga na kuchangia NSSF. Tunataka wajenge utamaduni wa kujiwekea akiba ili wawe na usalama wa maisha yao ya sasa na ya baadaye," alisema Bw. Kisaka.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Uwezeshaji Wanawake Tanzania (TAWEN), Florence Massunga, aliwataka wananchi waliojiajiri kuitumia fursa hiyo kujiunga na NSSF, akisema kufanya hivyo kutawasaidia kujenga usalama wa kifedha na kupunguza utegemezi wanapokumbwa na changamoto za maisha.

Baada ya ufunguzi wa shughuli hiyo, wananchi waliojiajiri walipewa elimu kuhusu mfumo wa hifadhi ya jamii, utaratibu wa kujiunga na kuchangia NSSF, mafao mbalimbali yanayotolewa na Mfuko pamoja na umuhimu wa kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba mapema ili kuwa na uhakika wa maisha ya sasa na baadaye.

Siku Maalumu ya Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi Waliojiajiri ni sehemu ya shughuli za NSSF katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, zenye lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi, kuongeza uelewa kuhusu hifadhi ya jamii na kuwahamasisha wananchi waliojiajiri kujiunga na kuchangia NSSF.




















No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad