Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ameitaka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuharakisha mchakato wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili iendane na mabadiliko ya sasa na kugusa kada zote nyeti zinazoshiriki kufanya maamuzi muhimu serikalini.
Kihenzile alisema hayo alipotembelea banda la Sekretarieti ya Maadili katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Dar es Salaam.
Alisema pamoja na Sheria ya Maadili ya mwaka 1995 kubainisha viongozi wanaopaswa kuzingatia masharti yake, bado kuna watumishi wengi wa umma wanaoshughulikia maamuzi nyeti lakini hawapo ndani ya wigo wa sheria hiyo.
"Sekretarieti ya Maadili inapaswa kuharakisha mabadiliko ya sheria ili izifikie kada zote nyeti. Kuna watumishi ambao si viongozi kwa mujibu wa sheria, lakini wanafanya maamuzi nyeti kuliko hata mimi kama Mbunge, mfano waliopo bandarini," alisema Kihenzile.
Naye mwananchi aliyefika katika banda hilo, Samson Alphonce aliishauri Sekretarieti ya Maadili kupanua utoaji wa elimu kwa kuwafikia viongozi wote kuanzia ngazi ya kitongoji hadi viongozi wa taasisi za umma na binafsi.
Alisema elimu ya maadili ikitolewa kwa wananchi kuanzia ngazi za chini itasaidia kuongeza uelewa kuhusu majukumu ya Sekretarieti ya Maadili, kuimarisha uwazi na kuwajengea wananchi imani katika mifumo ya uwajibikaji.
"Mimi sikuwa najua kuwa kuna Baraza la Maadili linalosikiliza mashauri ya viongozi wanaokiuka maadili kama ilivyo mahakama. Mitaani wengi tunafahamu mabaraza ya ardhi pekee. Elimu ikiendelea kutolewa, wananchi wengi wataelewa zaidi kazi za taasisi hii," alisema Manyamama.
Kwa upande wake, Afisa Maadili, Grace Matunda, alisema kwa sasa Sekretarieti inaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995, ambayo inawahusu viongozi waliotajwa na sheria hiyo.
Aliongeza kuwa pamoja na jukumu hilo, taasisi imeongeza juhudi za kutoa elimu ya maadili kwa wananchi kupitia mikutano ya vijiji, huku pia ikifundisha somo la maadili shuleni na kuanzisha klabu za maadili kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu.
Alisema hatua hizo zinalenga kujenga jamii inayozingatia maadili, uwajibikaji na uadilifu, sambamba na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu wajibu wa viongozi wa umma na nafasi ya Sekretarieti katika kusimamia maadili nchini.
.jpeg)
.jpeg)


No comments:
Post a Comment