JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Kafulila: Ubia si hiari, ni mkakati wa kuikomboa nchi kiuchumi

Share This

 


Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP-CENTRE), David Kafulila, amesema kuwa mfumo wa ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) si jambo la hiari au la kufikirika tu, bali ni mkakati madhubuti wa kimfumo unaolenga kuikomboa nchi kiuchumi na kuongeza ufanisi wa utendaji katika sekta mbalimbali.

Kafulila alibainisha hayo Alhamisi, Julai 30, 2026, wakati akihutubia wataalamu, wasomi, na wadau wa usafirishaji katika Kongamano la Mwaka la Chama cha Wataalamu wa Lojistiki na Usafirishaji Tanzania (CILT), lililofanyika katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Mabibo jijini Dar es Salaam.

Akichambua umuhimu wa mfumo huo, Kafulila alieleza kuwa mataifa mengi duniani yanageukia mifumo ya ubia kwa sababu kuu tatu ambazo ni kuvuta mitaji kutoka sekta binafsi, kuingiza teknolojia ya kisasa, na kuimarisha ufanisi wa usimamizi (management efficiency).

Alisisitiza kuwa uchumi wa sasa unategemea zaidi maarifa na ujuzi kuliko rasilimali za asili pekee.

"Ushirikiano wa kiuchumi kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) si jambo la hiari au la kuota, bali ni mkakati wa makusudi na wa kimfumo wa kuikomboa nchi kiuchumi na kuongeza ufanisi wa utendaji,” alisema.

“Serikali haiwezi kujenga kila kitu kuanzia bandari, reli, barabara, masoko na stendi, na wakati huo huo ikawa na fedha za kujenga watu wenye ubora wa kushindana duniani," aliongea.

Alibainisha kuwa kupitia PPP, serikali inajipa nafasi ya kuachia sekta binafsi maeneo ya kibiashara ili kuokoa fedha ambazo zinatumika kwenye uwekezaji mkubwa wa rasilimali watu kupitia elimu bora.

Katika kongamano hilo, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, alijibu ombi la Mkuu wa Chuo cha NIT, Dk Prosper Mgaya, kuhusu changamoto ya ukosefu wa mikopo kwa wanafunzi wanaochukua kozi za muda mfupi za kiufundi.

Dk Nchemba aliwahakikishia washiriki kuwa serikali imepokea ombi hilo kwa uzito mkubwa, akisema kuwa utaalamu katika fani za lojistiki na ufundi ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

"Serikali imepokea kwa uzito changamoto hiyo. Kozi za ufundi na lojistiki zinahitaji utimamu wa akili na uwezo wa mwanafunzi bila kujali hali ya kiuchumi ya familia anayotoka,” alisema Dk Nchemba.

“Serikali itaangalia mbinu mbadala ya kuwatengenezea mfumo rafiki wanafunzi wa kozi hizo za ufundi ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo," alisisitia.
Dkt. Nchemba alitolea mfano wa mfumo wa Samia Scholarship ambao umekuwa ukizingatia ufaulu na uwezo wa kitaaluma badala ya kigezo cha umaskini pekee, akiahidi kuwa serikali itaendelea kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu ya ufundi nchini.

Kongamano hilo limeonekana kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha sekta ya usafirishaji na mikakati mipana ya kiuchumi ya nchi kwa miaka 25 ijayo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad