JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


HATIFUNGANI YA iTRUST YAVUNJA REKODI YA MAFANIKIO KULIKO HATIFUNGANI ZOTE

Share This


OFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA. Nicodemus Mkama amesema mafanikio ya asilimia 760.78, yameifanya Hatifungani ya iTrust kuweka historia ya kuwa Hatifungani iliyopata mafanikio makubwa zaidi kupita hatifungani zote zilizowahi kutolewa hapa nchini. 

Amesema hatifungani iliyokuwa inashikilia rekodi hiyo, ni Hatifungani ya kampuni ya First Housing Finance Limited yaani MAKAZI Bond ambayo ilipata mafanikio ya asilimia 661.1 na kuorodheshwa kwenye Soko la Hisa tarehe 09 Juni 2026 huku akiipongeza iTrust kwa kuvunja rekodi na kuendelea kuweka rekodi za mafanikio katika masoko ya mitaji.

CPA.Mkama ameyasema hayo leo Julai 8,2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa Hatifungani ya Kampuni ya iTRUST Finance Limited katika Soka la Hisa Dar es Salaam 

“Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) pamoja na wadau wote wa sekta ya masoko ya mitaji tumefurahishwa sana na hatua hii, na tunatoa pongezi za dhati kwa Bodi na Menejimenti ya iTrust Finance Limited, wataalamu wote waliohusika kwa kuweka rekodi hii ya kihistoria.”

Amesema iTrust Finance Limited imeendelea kuwa mfano bora na wa kuigwa kwa kampuni na taasisi katika sekta ya umma na binafsi, kwani kampuni hiyo imekuwa ikitumia vizuri fursa zinazopatikana katika masoko ya mitaji kupata rasilimali fedha za kukuza na kuendeleza biashara; kuimarisha utendaji wa Kampuni; na kugharamia shughuli za maendeleo.

“Tangu mwaka 2021 (wakati huo kampuni hii ikitumia jina la Imaan Finance Limited) na hadi hivi sasa ikiwa na jina la iTrust Finance Limited, Kampuni hii imetumia fursa za masoko ya mitaji kwa njia ya utoaji wa Hatifungani, Sukuk na Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja.

Akifafanua zaidi amesema hatifungani hiyo ni ya kipekee na muhimu katika maendeleo na ustawi wa masoko ya mitaji, sio tu Tanzania, bali katika ukanda wa Afrika Mashariki, kwani hatifungani hii inaweka historia na rekodi kuu Tatu,

Amesema ni hatifungani ya kwanza (1) kuorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam, ikiwa imetolewa na kampuni yenye Leseni ya Uwakala wa Soko la Hisa (Licensed Broker/Dealer); na Leseni ya Usimamizi wa Mifuko ya Uwekezaji (Fund Manager) iliyotolewa na CMSA.

Pia ni hatifungani ambayo mauzo ya toleo la kwanza yameweza kuzidi kiasi cha Programu nzima ya Hatifungani yenye Thamani ya shilingi bilioni 100 zilizokuwa zitolewe katika awamu nne ndani ya miaka minne (bilioni 15, 20, 30 na 35, katika mwaka 2026, 2027, 2028 na 2029 mtawalia).

“Kama tulivyoshuhudia mauzo ya Hatifungani ya iTrust yamepata mafanikio ya asilimia 760.78, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 114.12 kimepatikana, ikilinganishwa na shilingi bilioni 15 zilizotarajiwa,”amesema.

Akieleza zaidi amesema mojawapo ya malengo ya DIRA ya Taifa ya Maendeleo (DIRA 2050) ni kuona kuwa Sekta ya Fedha, inawezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kukuza na kuendeleza biashara ambazo zinachangia ukuaji na ustawi wa sekta binafsi;

sekta ya umma na uchumi wa nchi kwa ujumla hapa nchini. 

“Hivyo basi, juhudi za iTrust Finance Limited zinatoa mchango katika utekelezaji wa malengo haya, na ni hatua madhubuti ya kuongeza fursa za uwekezaji katika masoko ya mitaji na kuleta matokeo chanya kwenye uchumi wa nchi yetu.”

Pia amesema kati ya wawekezaji waliowekeza kwenye hatifungani ya iTrust, asilimia 66.66 ni wawekezaji mmoja mmoja yaani Retail Investors na asilimia 33.34 ni Kampuni na Taasisi yaani Institutional investors . 

Aidha, asilimia 98.82 ni wawekezaji wa ndani na asilimia 1.18 ni wawekezaji wa kigeni huku akifafanua kuorodheshwa kwa hatifungani hiyo kunaongeza thamani ya uwekezaji katika Hatifungani za Kampuni na Taasisi kwa asilimia 5.46 na kufikia shilingi trilioni 2.20, kutoka shilingi trilioni 2.09. 

“Ushiriki mkubwa wa wawekezaji mmoja mmoja wa ndani ni hatua muhimu katika kuongeza ukwasi (liquidity) katika soko la hisa. Aidha, hii sehemu muhimu ya utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Huduma za Kifedha yaani National

Financial Inclusion Framework wenye lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye sekta rasmi ya fedha.

“Takribani asilimia 89 ya maombi yote ya uwekezaji kwenye Hatifungani ya iTrust

yamefanyika na kupokelewa kupitia mifumo ya kidijitali, ambapo mfumo wa kidijitali wa iTrust App pekee umechangia zaidi ya asilimia 71 ya maombi yote.”

CPA.Mkama amesema mafanikio hayo ni uthibitisho wa imani ya waliyonayo wawekezaji kwa Kampuni ya iTrust Finance Limited na masoko ya mitaji nchini. Aidha, mafanikio hayo ni matokeo ya mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na kiutendaji yanayotolewa na Serikali katika masoko ya mitaji. 




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad