JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Dubai na Tanzania Kuimarisha Ushirikiano wa Utalii na Biashara

Share This
Na Karama Kenyunko Michuzi Blog
DUBAI imeeleza dhamira ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika sekta ya utalii kupitia ushirikiano na waendesha utalii, mawakala wa safari na mashirika ya ndege ili kuongeza idadi ya Watanzania wanaotembelea jiji hilo pamoja na kunufaika na fursa za biashara na uwekezaji.

Akizungumza leo Julai 9, 2026 wakati wa maonesho ya kibiashara ya utalii jijini Dar es Salaam yaliyokwenda sanjari na kueleza mkakati mpya kwa wasafiri, wafanyabiashara, na watalii kutoka Tanzania kwenda Dubai, meneja msaidizi wa Operesheni za Kimataifa wa Shirika la Dubai la Utalii na Masoko ya Biashara (DCTCM), Khalaf Alaleeli, amesema ziara hiyo imelenga kuimarisha ushirikiano na wadau wa utalii nchini Tanzania na kuonesha fursa mbalimbali zinazopatikana Dubai.

Amesema Tanzania ni soko muhimu kwa Dubai kutokana na uhusiano wa safari, biashara na utamaduni kati ya nchi hizo mbili, huku ongezeko la Watanzania wanaosafiri nje ya nchi likichangiwa na urahisi wa kufika Dubai na huduma zinazotoa thamani ya fedha kwa familia, wafanyabiashara, vijana wataalamu na makundi mengine ya wasafiri.

Alaleeli amesema mwaka 2025 bara la Afrika lilichangia wageni 897,000 waliotembelea Dubai, sawa na asilimia tano ya wageni wote wa kimataifa, huku Tanzania ikiendelea kuwa sehemu muhimu ya mafanikio hayo.

Ameongeza kuwa kwa sasa kuna safari 33 za moja kwa moja kila wiki kutoka Dar es Salaam na Zanzibar kwenda Dubai, hatua inayorahisisha safari kati ya pande hizo mbili.

Amesema DET inaendelea kushirikiana kwa karibu na waendesha utalii, mashirika ya ndege na mawakala wa safari nchini Tanzania kwa kuwapatia taarifa za vivutio vipya, ofa za msimu na maarifa yatakayowawezesha kuandaa vifurushi vinavyokidhi mahitaji ya makundi mbalimbali ya wasafiri.

Alaleeli amesema mbali na utalii, Dubai inaendelea kujijenga kama kitovu cha biashara, usafirishaji na uwekezaji, jambo linalowapa Watanzania fursa ya kuitumia kama lango la kufikia masoko ya kikanda na kimataifa huku wakichanganya safari za biashara na burudani.

"Watanzania wanaotembelea Dubai watanufaika na vivutio vipya, migahawa inayotoa vyakula kutoka mataifa mbalimbali kwa gharama zinazokidhi bajeti tofauti pamoja na matukio mbalimbali yatakayofanyika mwaka 2026. Amesema Alaleeli

Aidha, amesema Dubai inaendelea kuweka kipaumbele katika usalama wa wakazi na wageni, huku huduma za hoteli, vivutio vya utalii, biashara na usafiri zikiendelea kutolewa kama kawaida.

Amewahamasisha Watanzania kuendelea kuichagua Dubai kwa safari zao, akisema jiji hilo liko karibu zaidi kuliko wengi wanavyodhani na linatoa mchanganyiko wa usalama, ukarimu, ununuzi, utamaduni, burudani, fukwe, shughuli za jangwani na huduma zinazokidhi mahitaji ya kila msafiri..

Katika maonesho hayo wadau zaidi ya 130 wa sekta ya usafiri na utalii, wakiwemo mawakala wa usafiri, waendeshaji wa ziara za utalii (tour operators), na mashirika ya ndege wamekutana
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DET Kanda ya Afrika, CIS na Ulaya ya Kati na Mashariki, Milo Radonjic amesema, maonesho ya mwaka huu ni fursa ya kuthibitisha dhamira yao katika soko la Tanzania na kuimarisha ushirikiano na sekta ya usafiri.

"Dubai inatoa huduma inayoendana na kila bajeti akibainisha kwamba utafiti uliofanywa na DET unaonesha kuwa wasafiri wengi wa Kitanzania Dubai kwa sasa wanazidi kutafuta maeneo ya likizo na biashara yenye unafuu wa gharama, wasaa mzuri wa kifamilia, maeneo ya ununuzi (shopping), utamaduni, na burudani katika eneo moja.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad