JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


DET YAFANYA MKUTANO WA BIASHARA YA UTALII DAR ES salaam

Share This

 

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
IDARA ya Uchumi na Utalii ya Dubai (DET) imefanya mkutano wake wa kila mwaka wa biashara ya utalii jijini Dar es Salaam, ukiwakutanisha mawakala 130 wa safari, waendeshaji wa utalii, mashirika ya ndege na wadau wa sekta ya utalii kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na sekta ya usafiri nchini Tanzania pamoja na kutangaza vivutio vipya vinavyopatikana kwa watalii wanaotembelea Dubai.

Mkutano huo ni sehemu ya mkakati wa DET wa kuendelea kushirikiana na soko la Afrika Mashariki, ambalo linaendelea kukua kwa kasi katika safari za kimataifa.

Kwa mujibu wa DET, Tanzania ni miongoni mwa masoko muhimu ya utalii barani Afrika kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya safari za kimataifa, mahusiano mazuri ya kibiashara pamoja na uwepo wa safari nyingi za moja kwa moja za ndege kati ya Tanzania na Dubai.

Takwimu za DET zinaonesha kuwa mwaka 2025 bara la Afrika lilichangia takribani wageni 897,000 waliotembelea Dubai, sawa na asilimia tano ya wageni wote wa kimataifa waliofika jijini humo, huku Tanzania ikiendelea kuwa miongoni mwa nchi zinazochangia ongezeko hilo.

Wasafiri kutoka Tanzania pia wananufaika na safari 33 za moja kwa moja kila wiki kutoka Dar es Salaam na Zanzibar kwenda Dubai, hali inayoufanya mji huo kuwa miongoni mwa maeneo rahisi kufikika kwa wasafiri wa Tanzania.

DET imeeleza kuwa Watanzania wengi sasa wanapendelea kutembelea maeneo yanayotoa huduma nafuu, burudani za familia, ununuzi, utamaduni na vivutio mbalimbali katika eneo moja.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Meneja Msaidizi wa Operesheni za Kimataifa wa Dubai Corporation for Tourism and Commerce Marketing (DCTCM), Khalaf Alaleeli, alisema mkutano huo unadhihirisha dhamira ya Dubai ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na sekta ya usafiri nchini Tanzania.

Alisema Dubai inaendelea kuwakaribisha wageni kwa kutoa huduma zenye thamani kubwa, vivutio vya kiwango cha kimataifa na uzoefu unaokidhi mahitaji ya kila aina ya msafiri, wakiwemo familia, wasafiri binafsi, makundi pamoja na wasafiri wa kibiashara.

Kwa mujibu wa DET, Dubai imeendelea kupanua huduma zake za utalii kwa kuongeza malazi yenye gharama nafuu, vivutio vya bure na vya gharama ndogo, maeneo mapya ya burudani kwa familia pamoja na moja ya miji yenye migahawa mingi na tofauti zaidi duniani, ikiwa na zaidi ya migahawa 13,000.

Aidha, Dubai imekuwa jiji la kwanza katika Ukanda wa Mashariki wa Dunia kutambuliwa kama Certified Autism Destination, hatua inayodhihirisha dhamira yake ya kuhakikisha utalii unakuwa jumuishi na unaowafaa watu wenye mahitaji maalumu.

DET imeeleza pia kuwa Dubai inaendelea kuwa miongoni mwa miji salama zaidi duniani kwa watalii, huku miundombinu ya utalii, hoteli, vivutio na huduma za umma zikiendelea kufanya kazi kwa kawaida.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad