Busan, Korea Kusini – Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika UNESCO, Mhe. Saidi Yakubu, amekutana na Waziri wa Nchi wa Japan anayeshughulikia Mambo ya Nje, Mheshimiwa Iwao Horii, pembezoni mwa Mkutano wa 48 wa Kamati ya Urithi wa Dunia unaoendelea jijini Busan, Korea Kusini.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Horii aliambatana na Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Japan katika UNESCO, Mhe. Takehiro Kano, ambapo pande hizo mbili zilijadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Japan katika maeneo ya uhifadhi wa Urithi wa Dunia, utamaduni na maendeleo endelevu kupitia UNESCO.
Mhe. Balozi Yakubu alitoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Japan kwa mchango wake mkubwa katika kulinda na kuhifadhi urithi wa utamaduni nchini Tanzania, hususan kupitia ufadhili wa ukarabati wa Jumba la Sinema la Majestic mjini Zanzibar. Aidha, alimpongeza Japan kwa kuendelea kutoa msaada katika miradi mbalimbali ya uhifadhi wa maeneo ya Urithi wa Dunia barani Afrika, hatua inayochangia kulinda historia, utamaduni na urithi wa vizazi vijavyo.
Mazungumzo hayo pia yaligusia fursa za kupanua ushirikiano katika kujengea uwezo wataalamu wa urithi, kubadilishana uzoefu wa kitaalamu pamoja na kuendeleza miradi ya pamoja ya kuhifadhi na kuendeleza maeneo ya Urithi wa Dunia nchini Tanzania.
Katika kikao hicho, Mhe. Balozi Yakubu aliambatana na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Taifa ya UNESCO Tanzania, Profesa Hamisi Malebo, pamoja na maafisa wengine waandamizi wa ujumbe wa Serikali ya Tanzania unaoshiriki Mkutano wa 48 wa Kamati ya Urithi wa Dunia.
Mkutano huo unaendelea kujadili masuala muhimu yanayohusu ulinzi, uhifadhi na usimamizi endelevu wa maeneo ya Urithi wa Dunia, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kulinda urithi wa asili na wa utamaduni kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho..jpeg)



No comments:
Post a Comment