JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Wito kwa Watanzania Wabunifu Kuleta Mabadiliko Mifumo ya Chakula Kupitia IGNITE Challenge

Share This

Nchini Tanzania, wabunifu na wajasiriamali wanaendelea kubuni suluhisho mbalimbali ili kukabiliana na changamoto kubwa zinazoikabili mifumo ya chakula nchini, kuanzia uhaba wa maji unaoathiri uzalishaji wa chakula mpaka upatikanaji mdogo wa vyakula vyenye lishe kwa watoto wadogo.


  • Ili kusaidia kukuza na kuongeza uwezo wa suluhisho hizi zinazoongozwa na wabunifu wa ndani, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), kwa kushirikiana na StartHub Africa, limezindua IGNITE Challenge Tanzania 1.0 — shindano la ubunifu linalolenga kutambua na kusaidia biashara pamoja na wabunifu wenye uwezo mkubwa wanaofanyia kazi suluhisho endelevu za mifumo ya chakula.

    Shindano hili linaangazia maeneo mawili muhimu: suluhisho za matumizi bora ya maji katika uzalishaji wa chakula na vyakula vya nyongeza vyenye lishe kwa watoto wenye umri wa miezi 6 mpaka miezi 59.

    Mpango huu unazialika kampuni changa au ‘startups’, biashara ndogo na za kati, wabunifu, na taasisi mbalimbali kuendeleza suluhisho zinazoweza kukua na kutekelezeka kwa vitendo ili kuongeza ustahimilivu kwa jamii, kuimarisha mifumo ya chakula ya ndani, na kuongeza upatikanaji wa lishe.

    Kwa mujibu wa WFP Tanzania, lengo la shindano hili siyo tu kutambua mawazo ya kibunifu, bali pia kusaidia suluhisho zenye uhalisia wa kutekelezwa na kukua kwa kiwango kikubwa zaidi.

    Washiriki watakaochaguliwa watanufaika na mafunzo ya kitaalamu, msaada wa maendeleo ya biashara, fursa za kuunganishwa na wadau wa mfumo wa ubunifu, pamoja na ufadhili wa mpaka Dola za Kimarekani 40,000 (zaidi ya Shilingi Milioni 100 za Kitanzania) kwa ajili ya hatua ya awali ya ukuaji na kuimarisha ubunifu wao.

    Akizungumza kuhusu mpango huo, Mkuu wa Ubunifu wa WFP Tanzania, Tayamika Mattao, alisema IGNITE Challenge inaonesha umuhimu unaozidi kukua wa ubunifu unaoongozwa na wadau wa ndani katika kukabiliana na changamoto za mifumo ya chakula na mabadiliko ya tabianchi nchini Tanzania.

    “Nchini Tanzania tunaendelea kuona wabunifu wakibuni suluhisho zenye manufaa makubwa kwa jamii, hasa katika sekta za kilimo, lishe, na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Kupitia IGNITE Challenge, tunataka kutengeneza fursa kwa wabunifu hawa kupata msaada, ushirikiano, na rasilimali zinazohitajika ili kukuza mawazo yao na kuchangia katika kujenga mifumo ya chakula iliyo imara na endelevu zaidi,” alisema Bi. Mattao.

    Shindano hili linakuja katika kipindi ambacho Tanzania, kama ilivyo kwa mataifa mengi duniani, inaendelea kukabiliwa na athari zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi zinazoathiri mifumo ya uzalishaji wa chakula, sambamba na changamoto za lishe kwa makundi yaliyo hatarini, hasa watoto walio chini ya miaka mitano.

    Kwa wabunifu wanaoendeleza suluhisho za kilimo zinazotumia maji kwa ufanisi ili kuimarisha mifumo endelevu ya chakula katika shule na kambi za wakimbizi, kuboresha upatikanaji wa maji, kuongeza ufanisi wa umwagiliaji, pamoja na uzalishaji wa chakula unaozingatia mabadiliko ya tabianchi, IGNITE Challenge inatoa fursa ya kujaribu, kuboresha, na kukuza suluhisho zao kwa manufaa mapana zaidi.

    Vilevile, wazalishaji au wasambazaji wa vyakula wenye uwezo wa kuzalisha vyakula vyenye lishe kwa watoto wenye umri wa miezi 6 mpaka miezi 59 wanahamasishwa kutuma maombi yao ili kusaidia kuboresha matokeo ya lishe kwa watoto nchini Tanzania.

    Mpango huu pia unaonesha mwelekeo unaokua wa mifumo ya ubunifu inayoongozwa na wadau wa ndani, ambapo wajasiriamali, taasisi za utafiti, wadau wa maendeleo, pamoja na sekta binafsi wanashirikiana kutengeneza suluhisho zinazokidhi mahitaji halisi ya jamii.

    Kupitia shindano hili, WFP kwa kushirikiana na StartHub Africa inalenga kuimarisha mfumo wa kukuza ubunifu na kusaidia biashara zenye matumaini ya kuchangia mifumo endelevu na imara ya chakula nchini Tanzania.

    Maombi ya kushiriki kwenye shindano la IGNITE Challenge Tanzania 1.0 yamefunguliwa rasmi.

    Waombaji wanatakiwa kutuma maombi yao kabla ya Ijumaa, tarehe 12 Juni 2026, kupitia:

    Suluhisho za matumizi bora ya maji katika uzalishaji wa chakula, maombi yatumwe kupitia tovuti ya: www.starthubafrica.org/ignite


    Vyakula vya nyongeza vyenye lishe kwa watoto wenye umri wa miezi 6–59, maombi yatumwe kupitia tovuti ya: www.starthubafrica.org/ignite

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad