JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


WABUNGE WAIPONGEZA NSSF NA PSSSF KWA SKIMU YA WALIOJIAJIRI

Share This

Wabunge wameipongeza Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kuendelea kupanua wigo wa huduma za hifadhi ya jamii kupitia Skimu ya Hifadhi kwa Wananchi Waliojiajiri, wakisema mpango huo unatoa fursa kwa mamilioni ya Watanzania kunufaika na huduma za hifadhi ya jamii.

Aidha, wamepongeza uwekezaji uliofanywa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) katika Kiwanda cha Kimataifa cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro (KLICL), wakisema mradi huo una mchango mkubwa katika kukuza viwanda, kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na kutengeneza ajira.

Pongezi hizo zilitolewa jijini Dodoma wakati wa semina ya wabunge kuhusu Skimu ya Hifadhi kwa Wananchi Waliojiajiri na Mradi wa Kiwanda cha Kimataifa cha Bidhaa za Ngozi cha Kilimanjaro.

Akizungumza kwa niaba ya Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu, Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Daniel Sillo, aliipongeza NSSF pamoja na PSSSF kwa kuendelea kutoa elimu kwa wabunge kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na mifuko hiyo.

Mhe. Sillo alisema elimu hiyo ni muhimu kwa wabunge kwani itawawezesha kuwa mabalozi wa kuhamasisha wananchi katika majimbo yao kujiunga na mifumo ya hifadhi ya jamii na kufahamu uwekezaji unaofanywa na mifuko hiyo.

Baadhi ya wabunge walioshiriki semina hiyo, akiwemo Mhe. Said Salimu na Mhe. Rashid Shangazi, waliipongeza NSSF kwa juhudi zake za kuwafikia wananchi waliojiajiri na kuimarisha huduma za hifadhi ya jamii nchini.

Walisema skimu hiyo itasaidia kujenga utamaduni wa kuweka akiba, kuongeza usalama wa kipato na kuwapa wananchi waliojiajiri fursa ya kunufaika na huduma za hifadhi ya jamii.

Kwa upande wa uwekezaji wa PSSSF, wabunge Jackson Kiswaga na Rashid Shangazi waliipongeza PSSSF kwa uwekezaji kwenye kiwanda hicho, huku wakiishauri sekta binafsi ikaribushwe katika uendeshaji wa kiwanda ili kuongeza nguvu katika masoko na uzalishaji.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, alisema Serikali inaendelea kuimarisha huduma za hifadhi ya jamii kwa kuwajumuisha wananchi waliojiajiri, ambao kwa muda mrefu walikuwa nje ya mifumo rasmi ya hifadhi ya jamii licha ya mchango wao mkubwa katika uchumi wa taifa.

Kuhusu PSSSF, Mhe. Sangu alisema mradi wa kiwanda hicho unamilikiwa kwa ubia kati ya Mfuko huo na Jeshi la Magereza kupitia kampuni yake ya Prisons Corporation Sole (PCS) na kuwa umekuwa na manufaa makubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alisema mfuko huo unalenga kuandikisha wananchi waliojiajiri milioni 3.7 ifikapo Juni 2031 kupitia Skimu ya Hifadhi ya Jamii. Alisema takribani asilimia 85 ya nguvu kazi nchini, sawa na wananchi milioni 20.98 wenye uwezo wa kufanya kazi, wamejiajiri, jambo linaloifanya skimu hiyo kuwa nyenzo muhimu ya kuwafikia makundi mbalimbali ya wananchi.

Bw. Mshomba alisema wanachama wa skimu hiyo watanufaika na mafao mbalimbali yakiwemo pensheni ya uzee, mafao ya urithi, ulemavu, uzazi na matibabu. Alisema wananchi sasa wanaweza kujiunga, kuchangia na kufuatilia taarifa zao kwa njia za kidijitali kupitia simu za mkononi, huku kiwango cha chini cha mchango kikiwa shilingi 30,000 kwa mwezi.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Fortunatus Magambo, amesema kiwanda hicho kinazalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na kimekuwa na mchango mkubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla. 

Alisema kiwanda hicho kimeongeza ajira kwa wananchi, kimeboresha kipato cha wananchi hususan wafugaji kupitia upatikanaji wa soko la uhakika la ngozi, na kuchochea mnyororo wa thamani wa sekta ya mifugo nchini.

“Kiwanda chetu kinazalisha bidhaa zenye ubora mkubwa, kimeongeza ajira kwa wananchi na kimefungua soko la uhakika la ngozi kwa wafugaji wetu, jambo linalonufaisha jamii na taifa kwa ujumla,” alisema Bw. Magambo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad