JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


TANZANIA, UMOJA WA ULAYA NA UNCDF WAWEKA MIKAKATI YA KUFIKIA ASILIMIA 80 YA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA IFIKAPO MWAKA 2034

Share This

Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati, kwa msaada wa Umoja wa Ulaya (EU), wameandaa Kongamano la Kitaifa la Nishati Safi ya Kupikia la siku mbili lililoanza jijini Arusha jana, likiwakutanisha wadau wakuu wa nishati safi ya kupikia, wizara na taasisi za serikali, sekta binafsi, wafadhili, washirika wa maendeleo, asasi za kiraia, na watafiti, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kuharakisha mabadiliko kitaifa kuelekea katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.


Kongamano hilo la siku mbili lililozinduliwa rasmi na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, ambapo wadau walijadili fursa na mikakati ya kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kufikia lengo la asilimia 80 ya kaya kutumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya, UNCDF na wadau mbalimbali inaendelea kuimarisha jitihada za kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kupitia maboresho ya sera na mifumo ya udhibiti, kutafuta rasilimali fedha, kutoa elimu kwa jamii na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi.

Licha ya mafanikio yaliyopatikana, matumizi ya kuni na mkaa bado ndiyo chanzo kikuu cha nishati ya kupikia kwa kaya nyingi nchini. Kuongeza matumizi ya nishati safi ni muhimu katika kuboresha afya za wananchi, kulinda mazingira na kuwawezesha wanawake na vijana ambao huathirika zaidi na athari za matumizi ya nishati za asili.

Chini ya kaulimbiu "Kuendeleza Mustakabali wa Nishati Safi ya Kupikia Tanzania: Mafanikio, Ushirikiano na Njia za Kufikia Asilimia 80 ya Matumizi ifikapo 2034," mkutano huo ulionesha mafanikio yaliyofikiwa, kubaini changamoto zilizopo na kuweka mikakati mipya ya kuongeza matumizi ya nishati safi nchini. Wadau walisisitiza umuhimu wa uratibu na ushirikiano katika utekelezaji, pamoja na kuwepo kwa mifumo madhubuti ya ufuatiliaji na uwajibikaji ili kuhakikisha uwazi na matokeo yanayopimika.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, alisisitiza dhamira ya Serikali akisema Serikali ya Tanzania imejipanga kikamilifu kuhakikisha inafikia lengo la asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

“Mkutano huu umetuwezesha kuoanisha sera, mifumo ya ufadhili na mikakati ya ushirikishwaji wa jamii ili kuharakisha utekelezaji, nishati safi ya kupikia ni muhimu katika kulinda afya za wananchi, kuwawezesha wanawake na vijana, pamoja na kuhifadhi mazingira yetu," alisema.

Aidha, alieleza kuwa juhudi za Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi zimekuwa chachu ya mabadiliko, huku kampeni za kitaifa zinazosimamiwa na UNCDF zikisaidia kuongeza uelewa wa wananchi na kubadili mitazamo kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa za kupikia.

Naye Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bi. Christine Grau, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano, akibainisha kuwa, Umoja wa Ulaya umetenga euro milioni 30, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 92 za Kitanzania, kwa ajili ya kupanua upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, kuimarisha masoko ya nishati endelevu, kulinda rasilimali asili na kuzalisha fursa za kiuchumi.

“Huu ndio ufadhili mkubwa zaidi wa Umoja wa Ulaya katika sekta ya nishati safi ya kupikia katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ukiendana na mkakati wa Global Gateway unaolenga kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi, kuhimiza ubunifu na kuleta matokeo yenye tija”, akiongeza kuwa msaada huo ni sehemu ya mkakati mpana wa kikanda wa kukuza maendeleo ya sekta binafsi na kupanua matumizi ya nishati safi ya kupikia barani Afrika.

Mkutano huo umefanyika wakati Tanzania ikiendelea kushuhudia mafanikio katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034). Kwa mujibu wa ripoti ya mkakati huo, matumizi ya nishati safi ya kupikia yameongezeka kutoka asilimia 16 mwaka 2022 hadi asilimia 28.6 kufikia Machi 2026. Mafanikio hayo yamechangiwa na ruzuku ya mitungi ya gesi ya LPG, kupunguzwa kwa gharama za umeme, kuondolewa kwa baadhi ya kodi kwenye vifaa vya nishati safi ya kupikia pamoja na uwekezaji wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA), zaidi ya watu bilioni 2.3 duniani bado hawana huduma za nishati safi ya kupikia, huku Bara la Afrika likiwa na idadi kubwa zaidi. Hivyo, juhudi za Tanzania zinachangia si tu katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa, bali pia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuboresha afya za jamii na kuimarisha usawa wa kijinsia duniani.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mshauri Mkuu wa Masuala ya Ufundi wa UNCDF, Bw. Peter Malika alisema, UNCDF ina jukumu la kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya maendeleo ya jamii kwa kuondoa vikwazo vinavyokwamisha uwezo wa wananchi kumudu gharama, usambazaji wa bidhaa na upatikanaji wa mitaji kwa biashara.

“Kupitia programu ya CookFund, tunawezesha upatikanaji wa fedha, kujenga ushirikiano na kusaidia biashara na wabunifu kuhakikisha suluhisho za nishati safi ya kupikia zinawafikia Watanzania wote."

“Kupitia programu hii UNCDF imeendelea kutoa mitaji kwa biashara ndogo na za kati ili kusaidia upanuzi wa teknolojia za nishati safi ya kupikia, kuchochea ubunifu na kuongeza ajira”, aliongeza Bw. Malika.

Tangu kuanzishwa kwake, programu hiyo imetoa zaidi ya dola za Marekani milioni 11.2 kupitia ruzuku 102 kwa biashara ndogo na za kati, na kusaidia ajira takribani 27,000 nchini.

Programu hiyo imewezesha zaidi ya kaya 413,000 kupata huduma za nishati safi ya kupikia, zikiwanufaisha karibu watu milioni 1.94 nchini kote. Aidha, imeziwezesha biashara 961 na taasisi za umma 45, ikiwemo shule zinazotumia briketi, majiko ya umeme ya shinikizo (EPC), gesi ya LPG na nishati nyingine endelevu. Hatua hizi zimechangia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa huku zikiboresha ufanisi, usalama na ubora wa huduma za upishi katika taasisi.

Katika sekta ya elimu pekee, wanafunzi 62,105 kutoka wilaya 14 katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma na Mwanza wamenufaika na programu hiyo, hatua iliyobooresha mazingira ya kujifunzia na kupunguza madhara yatokanayo na moshi. Kwa ujumla, utekelezaji wa CookFund umechangia kupunguza zaidi ya tani milioni 3.8 za hewa ukaa (CO₂e), na hivyo kusaidia Tanzania kufikia malengo yake ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuonesha nguvu ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.

Mkutano huo umehitimishwa kwa Serikali, wafadhili na sekta binafsi kuthibitisha upya dhamira yao ya kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuhakikisha kila kaya nchini inanufaika na suluhisho salama, nafuu na endelevu za kupikia.


Naibu Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Salome Makamba (kushoto), akipokewa na Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), Bw. Peter Malika, kabla hajazindua Kongamano la Kitaifa siku mbili la Nishati Safi ya Kupikia, lililoanza jijini Arusha leo. Kongamano hilo likiwa na kauli mbiu, "Kuendeleza Mustakabali wa Nishati Safi ya Kupikia Tanzania: Mafanikio, Ushirikiano na Njia za Kufikia Asilimia 80 ya Matumizi ifikapo 2034," linaangazia umuhimu wa kuoanisha sera, ufadhili na mikakati ya ushirikishwaji wa jamii ili kuharakisha maendeleo. Kongamano hilo limeandaliwa na UNCDF kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, kupitia Wizara ya Nishati, kwa msaada wa Umoja wa Ulaya (EU). Wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia, Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay na kulia ni Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Polycarp Nkuyumba


Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), Bw. Peter Malika (wa pili kuia), akizungumza wakati wa Kongamano la Kitaifa la siku mbili la Nishati Safi ya Kupikia, lililoanza leo jijini Arusha. Kongamano hilo likiwa na kauli mbiu, "Kuendeleza Mustakabali wa Nishati Safi ya Kupikia Tanzania: Mafanikio, Ushirikiano na Njia za Kufikia Asilimia 80 ya Matumizi ifikapo 2034," linaangazia umuhimu wa kuoanisha sera, ufadhili na mikakati ya ushirikishwaji wa jamii ili kuharakisha maendeleo. Katikati ni Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba na wa pili kushoto ni Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU), nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bi. Christine Grau.


Naibu Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Salome Makamba, akizindua Kongamano la Kitaifa la siku mbili la Nishati Safi ya Kupikia, lililoanza leo jijini Arusha. Kongamano hilo likiwa na kauli mbiu, "Kuendeleza Mustakabali wa Nishati Safi ya Kupikia Tanzania: Mafanikio, Ushirikiano na Njia za Kufikia Asilimia 80 ya Matumizi ifikapo 2034," linaangazia umuhimu wa kuoanisha sera, ufadhili na mikakati ya ushirikishwaji wa jamii ili kuharakisha maendeleo.
Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bi. Christine Grau, akizungumza wakati wa Kongamano la Kitaifa la siku mbili la Nishati Safi ya Kupikia jijini Arusha leo. Kongamano hilo limeandaliwa na UNCDF kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, kupitia Wizara ya Nishati, kwa msaada wa EU.

Naibu Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Salome Makamba (wa tatu kutoka kushoto), akipewa maelezo kuhusu faida ya matumizi ya majiko bora ya kupikia na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Burnstove Manufacturing, Bi. Lucia Petro (kulia), wakati wa Kongamano la Kitaifa la Nishati Safi ya Kupikia jijini Arusha leo.

Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Kitaifa la siku mbili la Nishati Safi ya Kupikia, lililoanza leo jijini Arusha wakiwa katika kongamano hilo lililoandaliwa na Shirila la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, kupitia Wizara ya Nishati, kwa msaada wa Umoja wa Ulaya (EU).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad