Na Janeth Raphael MichuziTv
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema mafanikio ya utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 yatategemea uwepo wa taasisi za umma zenye ushindani, zinazoendeshwa kwa matumizi ya teknolojia na zinazopimwa kwa matokeo halisi ya utendaji badala ya mazoea ya kazi.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza katika hafla ya kupokea gawio kutoka kwa taasisi na mashirika ya umma iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Amesema Dira ya Taifa 2050 inalenga kujenga uchumi imara na shindani, hivyo ni muhimu taasisi za umma zisimamie kwa ufanisi rasilimali za taifa ili ziwe chachu ya maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi.
Kwa mujibu wa Rais Samia, mafanikio ya dira hiyo hayatatokana na uwepo wa sera pekee, bali yatategemea namna taasisi zinavyosimamia mitaji ya umma, kupunguza upotevu wa mali na kutumia rasilimali zilizopo kuzalisha fursa mpya za kiuchumi.
"Hatutaweza kujenga uchumi shindani kwa taasisi zinazofanya kazi kwa mazoea. Tunahitaji taasisi zinazopimwa kwa matokeo badala ya takwimu," alisema Rais Samia.
Amesisitiza kuwa Serikali inalenga kuwa na taasisi zinazowajibika, zenye uwezo wa kutumia teknolojia kuongeza ufanisi wa huduma, pamoja na kufungua nafasi zaidi za ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kupitia ubia wenye manufaa kwa pande zote.
Rais Samia pia amezitaka taasisi zote za umma kuhakikisha mipango yao ya kimkakati na utekelezaji wa shughuli za kila siku vinaendana na vipaumbele vya Dira ya Taifa 2050, ili malengo yaliyowekwa yaweze kufikiwa na kutoa matokeo yanayoonekana kwa wananchi.
Aidha, ameeleza kuwa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi unapaswa kuwa na manufaa kwa wadau wote, huku akisisitiza umuhimu wa Watanzania kunufaika moja kwa moja na fursa zinazotokana na miradi ya maendeleo inayotekelezwa kupitia ushirikiano huo.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ametoa wito kwa taasisi na mashirika ya umma kuendelea kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa rasilimali za umma ili kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi na kufanikisha azma ya Tanzania ya kufikia maendeleo endelevu kupitia Dira ya Taifa 2050.




No comments:
Post a Comment