Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Oryx Gas Tanzania imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi kama sehemu ya mchango wake katika uhifadhi wa mazingira, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia ambayo ni salama na rafiki kwa mazingira.
Hayo yamesemwa leo Mei 5,2026 na Meneja Masoko na Mauzo wa Oryx Gas Tanzania Shaban Fundi katika Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambapo wafanyakazi wa kampuni hiyo wamefanya usafi katika Soko la Kimataifa la Samaki Feri jijini Dar es Salaam ambapo pia kampuni hiyo imekabidhi vifaa vya kufanyia usafi katika soko hilo.
Fundi amesema kampuni hiyo imekuwa ikitekeleza shughuli mbalimbali nchini kwa lengo la kuhamasisha utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi.
“Mbali na kufanya usafi wa mazingira katika soko hilo, Oryx pia tumetoa vifaa vya usafi, vifaa vya kunawia mikono pamoja na vifaa vya kutupia taka ili kuboresha mazingira ya wafanyabiashara na wananchi wanaotembelea eneo hilo.
“Leo tupo hapa Soko la Feri kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kwa kufanya jambo tofauti. Tumeungana na wateja wetu katika kufanya usafi wa mazingira, kutoa vifaa vya usafi na kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kulinda mazingira yetu kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema Fundi.
Aidha, amesema soko hilo ni mfano mzuri wa mafanikio ya matumizi ya gesi badala ya kuni na mkaa, hatua ambayo imechangia kupunguza uharibifu wa mazingira na kuongeza usalama katika eneo hilo.
“Hapo awali matumizi ya kuni na mkaa yalikuwa makubwa sana, lakini sasa mazingira yameimarika, usafi umeongezeka na usalama umeimarika. Tunatoa mwito kwa wananchi kuendelea kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kutumia gesi ambayo ni salama, nafuu na rafiki kwa mazingira.”
Ameongeza Oryx Gas imeendelea kuhakikisha upatikanaji wa gesi unaimarika nchini kote, mijini na vijijini, ili wananchi wengi zaidi waweze kufaidika na nishati hiyo safi.
Kwa upande wake, Meneja wa Soko la Kimataifa la Samaki Feri Suleiman Mfinanga ameipongeza Oryx Gas kwa kuchagua soko hilo kuwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, huku akieleza hatua hiyo imeonyesha dhamira ya kweli ya kampuni hiyo katika kulinda mazingira na kuboresha shughuli za biashara.
Ameongeza soko hilo ni miongoni mwa masoko makubwa ya samaki nchini, hivyo uwekezaji uliofanywa wa miundombinu ya matumizi ya gesi umekuwa na manufaa makubwa kwa wafanyabiashara na mazingira kwa ujumla.
“Tunawashukuru sana Oryx kwa uwekezaji huu mkubwa wa nishati safi mlioufanya katika soko ambapo mlituwekea tanki kubwa na wafanyabiashara wakaunganishiwa gesi ya kupikia. Mradi huu umechangia kwa kiasi kikubwa kutekeleza sera ya taifa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuondoa changamoto zilizokuwa zikitokana na matumizi ya kuni na mkaa,” alisema.
Naye mfanyabiashara katika soko hilo, Mwanahawa Noel, amesema ujio wa Oryx na kampeni zake za mazingira umewapa hamasa wafanyabiashara kuendelea kudumisha usafi wa mazingira na kuvutia wageni zaidi katika soko hilo.
“Tunawapongeza kwa kutukumbuka na kuendelea kutuhamasisha kuweka mazingira safi. Hii inasaidia hata wageni kutoka maeneo mbalimbali na nchi jirani kufurahia mazingira mazuri wanapofika hapa,” amesema.
Kwa upande wake, mfanyabiashara mwingine, Shaibu Ulaya, amesema mradi wa gesi uliotekelezwa na Oryx umeleta mafanikio makubwa katika shughuli za biashara na kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyabiashara wa soko hilo.
Maadhimisho hayo yalitumika pia kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi katika kupunguza uharibifu wa mazingira, kulinda afya za wananchi na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.

.jpeg)



No comments:
Post a Comment