-Mauzo yake yafikia kiasi cha Sh. bilioni 33.08 ikilinganishwa na Sh.bilioni 5 zilizotarajiwa
Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV
MAUZO ya Hatifungani ya MAKAZI ya Kampuni ya First Housing Finance Limited yamepata mafanikio ya asilimia 661.1, ambapo kiasi cha Sh.bilioni 33.08 kimepatikana, ikilinganishwa na Sh.bilioni 5 zilizotarajiwa.
Hatua hiyo inaiwezesha First Housing Finance Limited kuongeza rasilimali fedha na ukwasi, ambao utatumika kutoa mikopo ya nyumba kwa lengo la kuboresha makazi ya wananchi na kuongeza uwekezaji katika Sekta ya Nyumba na Uendelezaji Makazi.

Hayo yameelezwa leo Juni 9,2026 jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA), CPA. Nicodemus Mkama wakati wa hafla ya kuoredheshwa kwa hatifungani ya MAKAZI (MAKAZI BOND) ya Kampuni ya First Housing Finance Limited katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.
Amesema ongezeko hilo la rasilimali fedha linatarajiwa kuiwezesha First Housing Finance Limited kuongeza ufanisi zaidi wa kutoa huduma itakayofikia makundi mengi zaidi ya wananchi kwa ujumla.
“Naufahamisha umma kuwa kati ya wawekezaji waliowekeza kwenye hatifungani ya MAKAZI, asilimia 96.63 ni wawekezaji mmoja mmoja na asilimia 3.37 ni Kampuni na Taasisi.Asilimia 96.03 ni wawekezaji wa ndani na asilimia 3.97 ni wawekezaji wa kigeni.

“Vile vile, kuorodheshwa kwa hatifungani hiyo kunaongeza thamani ya uwekezaji katika Hatifungani za Kampuni na Taasisi kwa asilimia 1.63 na kufikia Sh.trilioni 2.06, kutoka Sh.trilioni 2.03.”
Ameongeza pia ushiriki mkubwa wa wawekezaji mmoja mmoja wa ndani ni hatua muhimu katika kuongeza ukwasi (liquidity) katika soko la hisa. Aidha, hiyo ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Huduma za Kifedha wenye lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye sekta rasmi ya fedha.
CPA.Mkama amesema mauzo ya hatifungani hiyo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha 2020/21 – 2029/30 wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli na miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi.

Aidha, mauzo hayo yamewezesha utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambapo fedha zilizopatikana zitatumika kuchochea shughuli za ujenzi; kuongeza fursa za ajira kwa wananchi; kuimarisha upatikanaji na umiliki wa makazi bora na nafuu; pamoja na kuongeza ushiriki wa wananchi katika sekta rasmi ya fedha, hususan masoko ya mitaji.
“Kuorodheshwa kwa hatifungani ya MAKAZI kunatoa fursa kwa wawekezaji kuuza hatifungani zao pale watakapohitaji fedha kwa ajili ya matumizi mengine, na kuwapatia fursa wawekezaji wapya kununua hatifungani hizi.
.jpeg)
“Uorodheshwaji wa hatifungani katika Soko la Hisa unawawezesha wawekezaji kujua thamani halisi ya hatifungani zao (Price Discovery); ambapo wawekazaji hao watapata faida ya uwekezaji wao (coupon payments).”
Ameongeza pia kuorodheshwa kwa hatifungani katika soko la hisa kunaimarisha utawala bora katika uendeshaji wa kampuni; na kumuwezesha mwekezaji kuwa na anuwai na hivyo hupunguza athari za uwekezaji (Diversification).
“Hivyo, tuna kila sababu ya kuipongeza First Housing Finance Limited pamoja na taasisi na wataalamu wote walioshiriki kuwezesha mafanikio haya. Ninatambua kazi hiyo haikuwa ndogo na rahisi lakini mmeweza kufanya kazi yenu vizuri na hivyo kufanikisha hatua hii kwa weledi na kwa ufanisi mkubwa.
“Mafanikio haya ni uthibitisho wa imani ya waliyonayo wawekezaji kwa Kampuni ya First Housing Finance na masoko ya mitaji nchini. Aidha, mafanikio haya ni matokeo ya mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na kiutendaji yanayotolewa na Serikali katika masoko ya mitaji,”amesema CPA Mkama.
Aidha amefafanua pia mojawapo ya malengo ya DIRA 2050 ni kuona kuwa Sekta ya Fedha inawezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kukuza na kuendeleza biashara ambazo zinachangia ukuaji na ustawi wa sekta binafsi; umma na uchumi wa nchi kwa ujumla.
“Hatifungani ya MAKAZI imetoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa malengo haya, na ni hatua madhubuti ya kuongeza fursa za uwekezaji katika masoko ya mitaji na kuleta matokeo chanya kwenye uchumi wa nchi yetu,”amesema.
.jpeg)




No comments:
Post a Comment