Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete akiongoza Mkutano huo wa Bodi ya GPE.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya GPE Dkt. Jakaya Kikwete akiwa na viongozi wa Taasisi hiyo wakati wa Mkutano huo wa Bodi. Wa kwanza kushoto ni Bw. Charles North, Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa GPE anayetokea Marekani, Bi. Christine Hogan, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya GPE anayetokea Canada, na kulia kwake ni Bi. Laura Frigenti, Afisa Mtendaji Mkuu anayetokea Italia.
RAIS Mstaafu Jakaya Dkt. Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE) ameendelea kuwa kinara katika kuhamasisha jitihada za upatikanaji wa fedha za kugharamia elimu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu duniani.
Kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bodi ya GPE ameongoza Mkutano muhimu wa Bodi hiyo uliofanyika Paris, Ufaransa tarehe 3 - 4 Juni, 2025 ambao pamoja na mambo mengine umejadili mkakati wa GPE kukusanya kiasi cha Dola za Marekani bilioni 15 hadi kufikia mwaka 2030 chini ya Kampeni ijulikanayo kama GPE 2030. Mkutano huo wa Bodi ulihudhuriwa pia na Bi. Éléonore Caroit, Waziri wa Nchi wa Ufaransa anayeshughulikia masuala ya Ubia wa Kimataifa na Maslahi ya Wafaransa waishio Ng'ambo.
Kupitia ubia na ushirikiano kati ya Taasisi ya GPE, nchi wafadhili, mashirika ya kimataifa ya misaada, GPE imelenga kuwarejesha watoto takriban milioni 270 ambao hawapo mashuleni kote duniani, hususan kutokana na sababu mbalimbali. Aidha, fedha zinazokusanywa na GPE hutumika pia kugharamia uboreshaji wa elimu ya awali na ya msingi kwa watoto wanaoishi katika nchi za kipato cha chini na zinazoendelea, hususan watoto wa kike na wale wanaojikuta kwenye mazingira magumu kama vile ya vita, ukame, mafuriko, nk.
Kupitia Kampeni hiyo ya GPE 2030, jumla ya wanafunzi milioni 750 kutoka katika nchi 96 kote duniani watanufaika kupitia uboreshwaji wa mifumo ya elimu, ununuzi wa vitabu vya ziada na kiada, ujenzi na uboreshwaji wa madarasa, maabara, na mafunzo kwa walimu na kuwaongezea ujuzi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Taasisi ya GPE baada ya Mkutano huo wa Bodi, nchi za Italia na Nigeria ndiyo zitaongoza Kampeni ya kukusanya fedha hizo katika hafla maalumu itakayofanyika tarehe 23 Septemba, 2026 pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA).
Vilevile, taarifa hiyo imeeleza kuwa licha ya mabadiliko ya sasa ya hali ya kifedha duniani ambapo wafadhili mbalimbali, hususan nchi zilizoendelea, zinabadilisha vipaumbele vyao vya maeneo ya kuelekeza ufadhili, Taasisi ya GPE imeridhishwa na mwitikio mzuri wa nchi wafadhili kama vile Ujerumani, Australia, Ufaransa, nk ambazo tayari zimetangaza michango yao kwa kampeni hiyo. Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa ni matarajio ya GPE elimu ya msingi itaendelea kuwa kipaumbele katika kipindi hiki cha mpito, huku Taasisi hiyo ikiahidi kuwa Taasisi ya mfano wa kuigwa wa ubia na ushirikiano wa kimataifa kwa kuzileta nchi pamoja kupitia lengo la kuboresha elimu ya msingi duniani.
Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Said Yakubu alihudhuria katika hafla iliyoandaliwa baada ya Mkutano huo. Ikumbukwe kuwa Tanzania ni moja ya nchi wanufaika wa fedha zinazotolewa na Taasisi ya GPE ambapo hadi sasa imeshapokea zaidi ya Dola za Marekani milioni 207.3 kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu nchini. Aidha, GPE imetenga takriban Dola za Marekani milioni 50 kwa ajili ya Tanzania ikiwa ni mwendelezo wa kuboresha sekta hiyo muhimu.
.jpeg)

.jpeg)


No comments:
Post a Comment