
Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
SERIKALI ya Tanzania imesema iko tayari kuongeza uzalishaji wa bidhaa na kutumia fursa ya soko la China kufuatia hatua ya taifa hilo kuondoa ushuru kwa bidhaa zinazotoka nchi za Afrika.
Balozi wa Tanzania nchini China, Dkt. Suleiman Haji Suleiman, amesema hayo leo Juni 25,2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungungumza na waandishi wa habari kuhusu ushirikiano wa Tanzania na China ulipofikia na fursa mbali mbali zitokanazo na ushirikiano huo.
Amesema hatua hiyo inaipa Tanzania nafasi ya kuuza zaidi bidhaa zake katika soko la China bila kutozwa ushuru, mradi bidhaa hizo zikidhi sheria za biashara za China na zile za Jumuiya ya Umoja wa Mataifa.
Akizungumzia mwenendo wa biashara kati ya Tanzania na China, Balozi Suleiman alisema kati ya mwaka 2021 na 2025 thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili imefikia Dola za Marekani bilioni 23.2.
Alisema kati ya kiasi hicho, Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.8 pekee, sawa na asilimia nane, huku bidhaa zilizoagizwa kutoka China zikifikia Dola za Marekani bilioni 21.3.
Alieleza kuwa pengo hilo linasababishwa na uzalishaji mdogo pamoja na kuendelea kuuza bidhaa ghafi bila kuziongezea thamani kabla ya kuzipeleka katika masoko ya kimataifa.
“Kwa mfano tunapeleka korosho ghafi China, wao wanazifungasha vizuri na kuziongezea thamani, kisha bidhaa hizo zinarejea tena sokoni. Kuna haja ya sisi kuongeza thamani bidhaa zetu hapa nchini kabla ya kuzipeleka nje,” alisema.
Balozi Suleiman alisema ubalozi unaendelea kutafuta fursa zaidi za uwekezaji kutoka China, hususan katika sekta za teknolojia, viwanda na upatikanaji wa mitambo ya kisasa ya uzalishaji ili kusaidia azma ya serikali ya kukuza uchumi wa viwanda.
Alisema makampuni mbalimbali kutoka China tayari yameonesha nia ya kuwekeza nchini, hatua ambayo inatarajiwa kuongeza ajira kwa Watanzania na kukuza uzalishaji wa ndani.
Wakati huo huo, Ubalozi wa Tanzania nchini China umetangaza kufungua kliniki maalumu ya biashara katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kwa lengo la kutoa ushauri wa moja kwa moja kwa Watanzania wanaotaka kuuza bidhaa katika soko la China au kuagiza mitambo kutoka nchini humo.
Alisema wataalamu kutoka ubalozini watakuwepo muda wote wa maonesho hayo kutoa elimu kuhusu bidhaa zinazohitajika katika soko la China, namna ya kusafirisha bidhaa, kupata vibali pamoja na fursa za uwekezaji na ununuzi wa mitambo ya viwandani.
“Lengo kuu ni kutoa huduma za ushauri kwa Watanzania kuelewa maana halisi ya soko la China, bidhaa gani unaweza kuzipeleka, namna ya kuzipeleka, sheria gani zinahitajika na namna ya kuomba vibali mbalimbali,” alisema.
Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kusukuma mbele diplomasia ya uchumi kwa lengo la kuongeza uzalishaji, ajira na mapato ya taifa kupitia biashara na uwekezaji.
“China siyo tu soko la bidhaa zetu, bali pia ni chanzo kikubwa cha teknolojia na mitambo inayoweza kusaidia maendeleo ya viwanda vyetu na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini,” alisema.






No comments:
Post a Comment