JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


BANK OF AFRICA TANZANIA YAIPONGEZA SERIKALI KWA BAJETI YA KUCHOCHEA UCHUMI

Share This

 

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji  Bank of Africa, Wasia Mushi ( wa pili kulia mstari wa pili, Mkuu wa Fedha Stivin Mwanjibili (wa pili kutoka kushoto mstari wa mwisho)   walijumuika na watendaji waandamizi wa taasisi nyingine kusikiliza hotuba ya Bajeti ya Kuu ya Serikali ya Mwaka 2026/2027 iliyosomwa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar,bungeni Dodoma mwishoni mwa wiki.


BANK Africa Tanzania imeipongeza Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2026/2027 yenye thamani ya shilingi trilioni 62.3, ikisema inalenga kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango wa Nne wa Maendeleo ya Taifa huku ikichochea ukuaji wa uchumi na uwekezaji nchini.

Benki hiyo pia imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuboresha huduma kwa wateja binafsi, wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) pamoja na makampuni makubwa ili kuunga mkono ajenda ya Serikali ya kuimarisha ushirikishwaji wa kifedha.

Akizungumzia bajeti hiyo iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, Dk. Khamis Mussa Omar, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bank of Africa Tanzania, Wasia Mushi, alisema bajeti ya mwaka huu imeweka mazingira mazuri kwa wawekezaji na wafanyabiashara kwa kuimarisha mageuzi ya kidijitali, kuvutia uwekezaji na kujenga uchumi himilivu na jumuishi.

“Kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji na biashara ni ishara kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kuleta mageuzi ya kiuchumi yanayowanufaisha Watanzania wengi zaidi,” alisema Mushi.

Alisema benki hiyo imevutiwa na hatua za Serikali za kuboresha mazingira ya biashara kupitia kupunguza urasimu, kurekebisha mfumo wa kodi na kuondoa migongano ya majukumu katika taasisi za umma.

Kwa mujibu wake, uwekezaji unaoendelea katika miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), barabara na nishati utaongeza mzunguko wa fedha, kuchochea shughuli za sekta binafsi na kuunda fursa zaidi za ajira.

Mushi alisema bajeti hiyo pia itasaidia kuvutia uwekezaji wa ndani na nje, kupanua wigo wa kodi, kuongeza ajira na kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari. Aidha, alibainisha kuwa Serikali imeendelea kutambua mchango wa sekta binafsi kama nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Aliongeza kuwa juhudi za kurasimisha sekta isiyo rasmi zitasaidia wafanyabiashara kupata masoko, huduma za kifedha, mikopo na bima, hatua itakayochochea zaidi ukuaji wa uchumi.

Mushi alisema Serikali imeendelea kutekeleza sera za fedha na bajeti zinazowezesha sekta binafsi kwa kuboresha mazingira ya biashara, kulinda thamani ya shilingi na kuongeza ukusanyaji wa mapato.

Kwa upande wa benki hiyo, alisema Bank of Africa Tanzania inaendelea kuwa imara kimtaji na kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia kanuni za mamlaka za usimamizi wa sekta ya fedha. Hivi karibuni benki hiyo imezindua tawi maalumu la wajasiriamali (SME Hub) pamoja na programu za huduma za kifedha na ushauri kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Alisema hatua hizo zinalenga kuboresha upatikanaji wa mikopo, kuongeza elimu ya biashara na kuimarisha ushindani wa kibiashara nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad