Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Mhe. Seif Kombo Pandu kushoto na Mkurugenzi wa Airtel Money Tanzania, Bw. Andrew Rugamba kulia wakipeana mikono na kubadilishana zawadi wakati wa kuzindua rasmi ushirikiano wa kimkakati wa "Airtel Money na ZECO – Tukuza Kidigitali" unaolenga kurahisisha malipo ya umeme visiwani humo. Uzinduzi huo umefanyika leo Zanzibar, Juni 2026.
Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Mhe. Seif Kombo Pandu, akihutubia wakati wa uzinduzi rasmi wa ushirikiano wa kimkakati wa "Airte

Mkurugenzi wa Airtel Money Tanzania, Bw. Andrew Rugamba, akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa ushirikiano wa kimkakati wa "Airtel Money na ZECO – Tukuza Kidigitali.", akisisitiza dhamira ya Airtel ya kuendelea kuleta urahisi na ufanisi wa huduma za kifedha kwa wananchi wa Zanzibar.
*Ushirikiano wa Airtel Money na ZECO kurahisisha malipo ya umeme wa TUKUZA visiwani humo.
*Waziri wa Nishati apongeza hatua hiyo akitaja kuwa itachochea Uchumi wa Bluu na maendeleo ya kidigitali.
*Benki ya PBZ yajipanga kuhakikisha ukwasi wa kutosha kwa mawakala ili kufanikisha miamala.
Zanzibar, Juni 2, 2026
KAMPUNI ya mawasiliano ya Airtel Tanzania, kupitia huduma yake ya Airtel Money, imeingia mkataba wa kimkakati na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kupitia mpango uitwao “Airtel Money na ZECO – Tukuza Kidigitali”.
Ushirikiano huu unalenga kuleta mageuzi makubwa katika ununuzi na malipo ya nishati ya umeme wa mfumo wa TUKUZA visiwani humo.
Kupitia mfumo huo mpya, wateja wa Airtel sasa wataweza kununua umeme wa TUKUZA kwa haraka, usalama na urahisi mkubwa kupitia simu zao za mkononi, mahali popote na wakati wowote, bila kulazmika kufika vituoni.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Mhe. Seif Kombo Pandu, ameupongeza ushirikiano huo akitaja kuwa ni hatua kubwa kuelekea uchumi wa kidigitali na kuboresha utoaji wa huduma za umma.
“Ushirikiano huu unaonesha dhamira yetu ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kisasa na zinazofikika kwa urahisi kupitia teknolojia. Umeme ni kichocheo kikuu cha uchumi wetu, ukisaidia sekta za utalii, afya, elimu, viwanda, pamoja na biashara ndogo na za kati (SMEs). Kila hatua inayorahisisha upatikanaji wake inachangia moja kwa moja katika maendeleo ya Zanzibar,” alisema Mhe. Pandu.
Naibu Waziri aliongeza kuwa mpango huo unaenda sambamba na malengo ya Sera ya Nishati Zanzibar ya mwaka 2025 pamoja na Mpango wa Maendeleo ya Nishati wa Miaka 15 (2025–2040), unaolenga kuimarisha usalama wa nishati na kupunguza gharama za uendeshaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Airtel Money Tanzania, Bw. Andrew Rugamba, alisema: “Kupitia ushirikiano huu na ZECO, wateja wa TUKUZA sasa wanaweza kurejesha nishati ya umeme kwenye makazi au biashara zao ndani ya sekunde chache tu. Huu ndio urahisi na ufanisi tunaotaka kuuleta kwa wananchi wa Zanzibar.”
Bw. Rugamba alibainisha kuwa, kupitia kampeni ya “Airtel Kila Kona”, kampuni hiyo imeendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa Zanzibar. Uwekezaji huo ni pamoja na kufungua vituo vipya vya huduma katika Mkoa wa Mjini Magharibi (eneo la ZSSF Mbweni) na kituo kikubwa cha kisasa katika Jengo la Muzammil, Mlandege.
Naye Meneja Mipango na Biashara wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) Bi. Aisha Omary, alifafanua kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa shirika hilo wa kutumia ubunifu wa kidigitali kuondokana na mifumo ya kizamani ya utoaji huduma. “Huu siyo tu urahisi wa malipo, bali ni hatua kubwa ya kujenga mfumo wa nishati wenye ufanisi na unaowajumuisha wananchi wengi zaidi,” alisema Bi. Omary.
Katika kuhakikisha huduma hiyo inasafiri bila vikwazo, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Bw. Arafat Ally Haji, aliahidi kuwa benki hiyo itahakikisha mawakala wote wa Airtel Money visiwani humo wanakuwa na ukwasi (float) wa kutosha wakati wote.
“Kupitia ushirikiano wetu na Airtel, PBZ itahakikisha miamala yote, ikiwemo ununuzi huu wa umeme wa TUKUZA, inafanyika kwa haraka na ufanisi wa hali ya juu bila kukwama kwa kukosekana kwa fedha mtandaoni,” alisisitiza Bw. Arafat.
Uzinduzi huu wa mpango wa “Airtel Money na ZECO – Tukuza Kidigitali” unadhihirisha nguvu ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) katika kuongeza ujumuishi wa kifedha na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.



No comments:
Post a Comment