JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Wastaafu wa TRA Waiomba Jamii Kushirikiana na Walezi wa Vituo vya Yatima

Share This

 




Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
JAMII imetakiwa kuguswa na kushiriki katika malezi ya watoto yatima pamoja na wale wenye mahitaji maalum wanaoishi katika vituo mbalimbali vya kulelea watoto, ili kuwapatia mazingira bora ya makuzi na maisha yenye matumaini.

Wito huo umetolewa na Umoja wa Wastaafu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati walipotembelea Makao ya Watoto Wetu Tanzania yaliyopo Mbezi pamoja na Kituo cha Watoto wenye Usonji cha Norca Upendo kilichopo Kimara jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya utaratibu wao wa kila mwaka wa kutoa misaada ya kijamii.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo ya upendo, mmoja wa wastaafu hao, George Israel, alisema jamii inapaswa kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye changamoto za usonji majumbani, badala yake iwapeleke katika vituo maalum vinavyoweza kuwasaidia kupata matibabu na malezi sahihi.

Aidha, aliwataka wananchi kuwaunga mkono walezi wa vituo hivyo kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali ili kuwatia moyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwalea watoto hao.

“Tumejionea mambo makubwa sana. Naiomba jamii iendelee kutoa misaada na kushirikiana na watu wenye maono haya ya kuwalea watoto wenye uhitaji,” alisema Israel.

Kwa upande wake, Mratibu wa ziara hiyo, Lukasi Kaigalula, alisema umoja huo umeendelea na utaratibu wa kujichanga kila mwaka kwa lengo la kuwasaidia watoto yatima na wale wanaolelewa katika mazingira magumu.

“Wastaafu tunajichanga na kuwaletea watoto hawa mahitaji mbalimbali. Kuna kila sababu ya kuwapa moyo wale wote waliojitolea kuwalea watoto hawa,” alisema Kaigalula.

Naye Catherine Mkelebe alitoa rai kwa jamii kupunguza migogoro ya kifamilia na ndoa, akisema hali hiyo imekuwa chanzo cha kuongezeka kwa watoto wanaokosa malezi ya wazazi au walezi.

“Migogoro ya ndoa si jambo zuri, kwani wanaoumia zaidi ni watoto. Tunawaasa wazazi watimize wajibu wao wa malezi ili kulinda ustawi wa watoto,” alisema.

Kwa upande wake, mlezi wa Kituo cha Norca Upendo, Grace Flavian Mauki, alisema kituo hicho kilianza kwa kulea watoto wawili pekee, lakini sasa kina watoto zaidi ya 50, hali inayoonyesha ukubwa wa changamoto hiyo katika jamii.

Alisisitiza kuwa watoto wenye usonji hawapaswi kufichwa majumbani, kwani wanaweza kusaidiwa kupitia mazoezi tiba na huduma maalum zinazotolewa katika vituo vya malezi.

“Tunaiomba jamii isiwafiche watoto hawa ndani. Wapelekwe kwenye vituo maalum kwa sababu wanaweza kusaidiwa na kupata maendeleo mazuri,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Makao ya Watoto Wetu Tanzania pamoja na Mwenyekiti wa Wamiliki wa Makao ya Watoto nchini, Evance Tegete, alisema kituo hicho kinajivunia kuwasaidia watoto waliotoka katika mazingira magumu hadi kufikia mafanikio makubwa ya kielimu na kijamii.

Alisema baadhi ya watoto waliowahi kulelewa katika makao hayo sasa ni wasomi na wananchi wenye mchango mkubwa katika jamii.

Wakihitimisha ziara yao, wastaafu hao walitoa wito kwa jamii kuendelea kuwalinda watoto, kuwathamini na kushiriki katika kuhakikisha wanapata malezi bora yatakayowawezesha kutimiza ndoto zao.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad