JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


WANANCHI WATAKIWA KUWATUNZA PUNDA KWA MANUFAA YA UCHUMI WA KAYA

Share This

 


Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
WANANCHI wametakiwa kuwathamini na kuwatunza Punda kwa kuhakikisha wanapatiwa huduma muhimu ili waweze kuendelea kuchangia katika kukuza uchumi wa kaya na jamii kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa na viongozi wa serikali pamoja na wadau wa ustawi wa wanyama wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Punda Duniani yaliyofanyika kitaifa katika Mtaa wa Mgusu, Manispaa ya Geita.

Imeelezwa kuwa punda ni miongoni mwa wanyama kazi wenye mchango mkubwa katika shughuli za kila siku za wananchi hasa katika maeneo ya vijijini ambako hutumika kusafirisha maji, kuni, mazao ya kilimo pamoja na vifaa vya ujenzi.

Kutokana na umuhimu huo, serikali imeendelea kuweka nguvu katika kulinda haki na ustawi wa mnyama huyo huku mamlaka zote za serikali zikiagizwa kuhakikisha zinasimamia kikamilifu sheria za ustawi wa wanyama ikiwemo punda pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya sheria watu wote wanaokiuka sheria hizo.

Serikali imesisitiza kuwa punda wanapaswa kupatiwa chakula, maji, matibabu na sehemu nzuri ya kulala kama ilivyo kwa mifugo mingine.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba amesema bado baadhi ya wananchi hawajatambua thamani ya punda na wamekuwa wakimtendea ukatili kwa kumbebesha mizigo mizito kupita kiasi na kutompatia huduma muhimu.

Amesema kupungua au kutoweka kwa punda kutakuwa na athari kubwa kwa wananchi wanaowategemea katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kwamba kazi nyingi zinazofanywa na punda zitakuwa mzigo mkubwa kwa wananchi endapo mnyama huyo hatalindwa na kutunzwa vizuri.

“Wananchi hawana budi kumtunza punda kwa sababu anawaingizia kipato, siku punda wakitoweka, kazi za kusomba mchanga, tofali, kubeba maji, kuni pamoja na kazi za mashambani zitafanywa na watu wenyewe jambo ambalo litapunguza uzalishaji na kipato kwa kaya,” amesema Hashim Komba.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesema ni vyema wananchi wakaanza kubadili mtazamo wao kwa kuhakikisha punda wanapata chakula, maji na sehemu salama ya kulala badala ya kuwaacha wakizagaa mitaani na barabarani nyakati za usiku jambo linaloweza kuhatarisha maisha yao.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad