📍Njombe
Mkoa wa Njombe umetangaza rasmi fursa mpya za uwekezaji katika sekta ya madini baada ya kubainika kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali za madini ambazo bado hazijatumika ipasavyo, huku wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wakialikwa kuwekeza katika utafiti, uchimbaji na uongezaji thamani wa madini hayo.
Wito huo umetolewa na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Lucas Mlekwa, wakati akizungumza katika mahojiano maalum na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma cha Tume ya Madini kinachoshiriki Kikao Kazi cha 21 cha Maafisa Habari, Mawasiliano, Itifaki na Uhusiano Serikalini kinachoendelea mkoani humo.
Mhandisi Mlekwa amesema tathmini za kitaalam zinaonesha kuwa wilaya za Njombe, Ludewa, Makete na Wanging’ombe zina utajiri mkubwa wa madini yenye thamani ya kiuchumi, licha ya mengi yake kutokuwa yameendelezwa kikamilifu.
Ametaja madini hayo kuwa ni pamoja na chuma, yanayotumika katika uzalishaji wa chuma cha pua na ujenzi wa miundombinu; manganese, muhimu katika utengenezaji wa chuma na teknolojia za kisasa za betri; pamoja na tantalite, madini mkakati yanayotumika katika vifaa vya kielektroniki kama simu za mkononi, kompyuta na vifaa tiba.
Aidha, amesema mkoa huo una vito mbalimbali vinavyotumika katika mapambo ya thamani, marumaru ya bluu kwa ajili ya ujenzi na mapambo ya majengo, pamoja na jiwe la amazonite linalohitajika katika soko la kimataifa la vito.
Madini mengine yaliyopo ni mica inayotumika katika vifaa vya umeme, teknolojia na vipodozi; shaba inayotumika katika mifumo ya umeme, nishati jadidifu na mashine za viwandani; pamoja na makaa ya mawe yanayochangia uzalishaji wa nishati na shughuli za viwanda.
Mhandisi Mlekwa pia amebainisha uwepo wa dhahabu, mojawapo ya madini muhimu ya biashara na akiba ya kifedha duniani, pamoja na madini adimu (rare earth elements) yanayotumika katika teknolojia za kisasa ikiwemo magari ya umeme, mitambo ya kuzalisha umeme wa upepo, smartphones na viwanda vya teknolojia ya juu.
“Tunawaalika wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika utafiti wa madini, uchimbaji, uongezaji thamani na ubia kuchangamkia fursa zilizopo mkoani Njombe,” amesema.
Ameeleza kuwa uwekezaji katika sekta hiyo utaongeza kasi ya ukuaji wa viwanda, utazalisha ajira kwa wananchi, utaongeza mapato ya Serikali na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika mnyororo wa thamani wa madini duniani.
Wakati huo huo, kikao kazi kinachoendelea Njombe kimewakutanisha maafisa habari, mawasiliano, itifaki na uhusiano serikalini kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa kitaaluma, kuimarisha ushirikiano na kuongeza ufanisi wa mawasiliano ya Serikali kwa umma.
Kikao hicho kinatarajiwa kuimarisha uratibu wa mawasiliano ya Serikali pamoja na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo mchango unaozidi kuongezeka wa sekta ya madini katika uchumi wa Taifa.
.jpeg)






No comments:
Post a Comment